Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Hongera JK kwa juhudi za kuokoa maisha ya kinamama wajawazito

22nd July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Rais Jakaya Kikwete, amejitoa kupambana na malaria pamoja na kupunguza vifo vya wanawake vinavyohusiana na uzazi na ujauzito

Mwaka jana shirika la wafanyabiashara wa Soko la Hisa la New York Marekani (NASDAQ) na Taasisi ya Umoja wa Mataifa zilimpongeza kwa juhudi za kupambana na changamoto hizo kwa kumpa tuzo, kila moja ikitoa tunzo yake.

Juhudi hizo za kuokoa maisha ya kinamama wajamzito na watoto zimetukuka tena mwaka huu pale Umoja wa Afrika huko Ethiopia wiki hii ulipompatia tunzo nyingine kwa jitihada za kupambana na changamoto za malaria na kuokoa maisha ya mama na mwana.

Tuzo hizo zote zinatokana na namna juhudi zake zinavyoonyekana kitaifa na kimataifa katika kuokoa maisha ya makundi hayo muhimu katika maendeleo ya taifa letu Tanzania.

Kwa dhati tunapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza kwa juhudi hizi ambazo sote yatupasa kuziunga mkono ili kuwa na taifa endelevu kwa vizazi vijavyo. Ushiriki wetu sote utakuwa chachu kwake katika kuhakikisha kuwa wanawake ambao ni wazazi wa wapiga kura, walipa kodi na nguvu kazi ya Tanzania hawapotezi maisha yao wala ya watoto wao.

Tunaelewa kuwa changamoto nyingi zipo vijijini hasa maeneo ambayo mila na desturi zinatawala na kupelekea mabinti kuozwa, kuwalazimisha wanawake kuolewa na wanawake wenzao nyumba ‘ntobu’ na nyumba ‘bhoke’, kuwatakasa wajane , na kuwapiga wajawazito.

Vile vile kukataa watoto na kuwabagua watoto wa kike na kuwathamini zaidi wavulana, mambo ambayo yamekuwa yakileta msongo wa mawazo na kuwapeleka wanawake ama kwenye ujauzito lakini usiotizama hatma ya uzazi salama ama kuwaua kwa mawazo na huzuni nyingi.

Wakati tukitafakari hayo, tunamwomba Rais Kikwete ahakikishe kuwa taifa linapata sheria za kupambana na ukatili wa kijinsia, ambao kwa kiasi kikubwa unachangia vifo vya wajawazito na watoto.

Katiba mpya ambayo wananchi wanatoa maoni yao hivi sasa ikataze ukatili wa kijinsia Tanzania kwa kutamka kuwa watu wote ni sawa bila kubagua jinsi zao.

Katiba mpya itamke kuwa hakuna kutunga sheria zinazokwenda kinyume na haki za raia, mfano sheria kandamizi dhidi ya wanawake na mabinti kama zile za kuwaoza mabinti wadogo, Katiba ikataze ndoa za watoto na kutangaza umri wa kuolewa kuwa ni kuanzia miaka 20 siyo vinginevyo.

Kuwe na jitihada za kuwaandaa mabinti kuwa majasiri mashuleni ili wasinyanyaswe kingoni na pia kuwajengea mazingira mashuleni kueleza matatizo yao na kutaja visa na vituko wanavyofanyiwa ili hatua dhidi ya watuhumiwa zichukuliwe mapema.

Itungwe sheria ya kuwalinda wajawazito na watoto, iwepo sheria inayokataza mila potofu na kutoa adhabu kali kwa wanaume ama jamii zinazoendeleza mila mbaya kuwatakasa wajane, kuwarithi na kuwapokonya mali za marehemu waume zao.

Pamoja na katiba mpya kuleta haki na faraja kwa wanawake, ni lazima kuwe na mikakati ya kuwalinda na kuwatibu wanaobakwa.

Wapatiwe tiba na ushauri nasaha ili wasiishie kujiua kutokana na udhalilishaji waliopitia. Pia kuwe na sheria za kuwashughulikia madaktari na wauguzi ambao wanawanyanyasa wajawazito na wazazi mahospitalini.

Wanawake wengi wanazalia majumbani kutokana na kusemwa ama kunyanyaswa na wahudumu mahospitalini. Wengine wanapoteza maisha kutokana na kucheleweshewa huduma.

Lakini pia ili kupunguza vifo ni lazima pia serikali iwafunze wahudumu wasaidizi hasa maeneo ya vijijini pamoja na kuwapa vifaa ili kuwasaidia wazazi na wajawazito hasa kwenye maeneo ambayo hakuna madaktari wala wakunga wa kutosha.

Wauguzi hawa wafanyiwe ushauri nasaha juu ya kupunguza misongo ya mawazo wanapowahudumia wazazi na wajawazito na pia wapewe matosha na vitendea kazi kwani kazi za ukunga na uzalishaji ni ngumu na zinachosha.

Ni imani yetu kwamba Rais wetu atayafanyia kazi yote hayo ili vifo vinavyotokea kwa uzembe viweze kuzuiwa na hivyo wanawake na watoto wajione salama wakati wote wanapohitaji huduma za afya mahospitalini, kwenye zahanati na vituo vya afya nchini

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment