


.jpg)
Mabingwa watetezi wa klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga wamepangwa kufungua dimba la michuano hiyo mwaka huu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye moja ya mechi mbili za ufunguzi itakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Jumamosi Julai 14.
Si tu timu za Burundi huwa ni wasindikizaji katika historia ya karibu miaka 40 ya Kombe la Kagame bali pia Atletico si moja ya majina yaliyozoeleka ya klabu za nchi hiyo.
Wawakilishi wengine wa Bara, mabingwa wa soka nchini Simba watacheza na URA ya Uganda Jumatatu Julai 16 kwenye Uwanja wa Taifa pia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, Katibu Mkuu wa Baraza la soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicolaus Musonye, alisema wawakilishi wengine wa Bara Azam FC na Mafunzo ya Zanzibar zitapambana zenyewe kwenye mchezo utakaochezwa Jumapili Julai 15 kwenye uwanja wa Azam Complex.
Musonye alisema mashindano ya mwaka huu yatashirikisha timu 10 kutoka katika nchi 10 wanachama wa CECAFA pamoja na timu moja mwalikwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
"Mwaka huu kuna nchi nne ambazo hazina mwakilishi katika mashindano haya na hii inatokana na sababu mbalimbali," alisema.
Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia hazitashiriki mashindano ya mwaka huu, alisema Musonye.
Alisema kwa wawakilishi wa Sudan, timu ya El Mereikh wameshindwa kushiriki mashindano ya m
aka huu kutokana na kukabiliwa na mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikisho na huku ligi kuu ya Sudan inaanza wiki ijayo.
Musonye alisema Somalia wameshindwa kushiriki kutokana na kuingia kwa uongozi mpya wa Chama cha soka cha nchi hiyo hali iliyopelekea kutoajipanga kwa wakati kushiriki mashindano ya mwaka huu.
"Eritrea tumewaondoa kutokana na matatizo ya mwaka jana, kwa hiyo hawatakuwa na mwakilishi kwenye mashindano ya mwaka huu," alisema Musonye.
Mwaka jana baadhi ya wachezaji wa Eritrea walifanya jaribio la kuzamia nchini baada ya kumalizika kwa mashindano.
Musonye alisema timu zinazoshiriki kwa mwaka huu zimepangwa kwenye makundi matatu ambapo Kundi A litakuwa na timu za Simba, URA, Vita Club (DRC) na Ports ya Djibout.
Kundi B litakuwa na timu za Azam FC, Mafunzo na Tusker ya Kenya, alisema wakati Kundi C litakuwa na timu za Yanga, APR (Rwanda), Wau Salaam (Sudan Kusini) na Atletico ya Burundi.
Aidha, alisema mdhamini mkuu wa mashindano hayo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameshakabidhi dola za Marekani 60,000 kwa ajili zawadi kwa bingwa wa mashindano hayo, mshindi wa pili na mshindi wa tatu.
Bingwa wa mshindano hayo atapewa dola 30,000, mshindi wa pili dola 20,000 wakati mshindi wa tatu atapata dola 10,000.
"Bado tunaendelea kutafuta wadhamini wa kufanikisha mashindano haya ambayo yanafanyika kwa mara nyingine hapa Tanzania," alisema.
"Mpaka sasa bado hatujafanikiwa kuwapata ila juhudi zinaendelea."
Mashindano hayo yatafikia mwisho Julai 28 kwa mchezo wa fainali utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.