



Imekuwa kama ada, kila uchao kuna jambo jipya linajitokeza kama moja ya changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwelekeo wa siku za hivi karibuni unatoa picha kwamba Muungano wa nchi hizi mbili ni kama umejengwa juu ya urafiki wa kutokuaminiana.
Inawezekana uhuru wa kutoa maoni kwa njia za uwazi zaidi umetoa fursa kwa watu wengi zaidi kuzungumzia kasoro zilizoko katika Muungano wa huu, hali ambayo miaka kabla ya 90 haikuwako.
Tunaamini kwamba watu kuwa na uhuru wa kuzungumzia Muungano na changamoto zake ni njia moja sahihi ya kujenga; kwa maana kwamba kama udhaifu ukijulikana na kuzungumzwa basi watu watakuwa tayari kutatua hitilafu hizo. Wahenga walisema kujua tatizo ni nusu ya kupata utatuzi wake.
Pamoja na changamoto zote zinazoweza kutajwa kuwa ni kero hasa za Muungano, uamuzi wa hivi karibuni wa kuwataka Watanzania wenye asili ya Bara kulipa kodi ya ardhi ya Dola za Marekani 5,000 kwa mwaka sawa na raia wengine wa kigeni, hakika ni kielelezo kwamba wapo watu wanaochokonoa kadri wawezavyo ili kuudhoofisha Muungano!
Maamuzi haya yanadaiwa kuwa yanatokana na sheria ya ardhi ya mwaka 1992 ya Zanzibar ambayo inamtaja Mzanzibari pekee kuwa na haki ya kumiliki ardhi visiwani humo, wengine wote wanahesabika kama wageni, yaani hata Watanzania wanaotoka Bara wanatambuliwa kama wageni!
Kutokana na sheria hiyo, Watanzania kutoka Bara waliolowea na kujiendeleza Zanzibar kwa miaka, wakapata kipande cha ardhi na kuiendeleza sasa watalazimika kulipa kodi hiyo kwa mwaka kama walivyo wageni wengine wowote kutoka kona yoyote ya dunia hii.
Haya yakitokea Zanzibar, sheria za ardhi namba nne na tano za Tanzania za mwaka 1998, zinahalalisha kila Mtanzania kuwa na haki ya kumiliki ardhi. Mtanzania huyu aweza kuwa yule wa kuzaliwa au wa kuomba; wote wanaruhusiwa kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kigezo hiki kinawapa hata Wazanzibari haki ya kumiliki ardhi Bara.
Tunatambua kwamba wapo Wazanzibari wengi tu wajasiriamali waliobobea wamejiendeleza na sasa wanamiliki si tu ardhi, bali mali za uhakika zisizohamishika Tanzania Bara. Hawa wana haki kabisa mbele ya sheria kumiliki wanachomiliki na kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi, sisi tunawatia shime wawekeze zaidi na zaidi kwa ajili ya ustawi wa nchi yao.
Lakini wakati tukitambua sheria na hali halisi ya ardhi kwa pande zote za Muungano, yaani Zanzibar yenye ardhi finyu na Tanzania Bara yenye ardhi kubwa na fursa nyingi, tunapatwa na wasiwasi kwamba kwa nini katika kipindi hiki ambacho Muungano unapita katika kipindi cha majaribu makubwa, suala la kuwaweka kundi moja Watanzania wa Bara kundi moja na wageni linawekewa mkakati?
Tunashindwa kujua kama kweli msukumo pekee wa kuwaweka Watanganyika katika kundi la wageni visiwani Zanzibar ni matokeo ya mahitaji ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya visiwa hivyo, au ni njia nyingine ya mapambano kama nyingine nyingi ambazo zimeshuhudiwa katika siku za hivi za karibuni za Zanzibar kutaka kujionyesha kwamba ni taifa linalojitegemea?
Tunasema haya si kwa sababu tunaunga mkono mbinu zozote mbaya za kukandamiza haki za Wazanzibari, ila tunasukumwa na kitu kimoja; kwamba baada ya miaka 45 ya Muungano kila uchao tofauti zinatafutwa, kukuzwa na kupigiwa mbiu kana kwamba kufanya hivyo ndiyo njia ya kuujenga.
Tunapata hofu kwamba kama viongozi wetu wasipokaa kitako na kutafakari kwa mapana mambo yanayotengenezwa, kusukumwa na kupigiwa kampeni kuhusu udhaifu wa Muungano, kuna kila dalili kwamba huko tuendako mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Tunafikiri huu si wakati wa kuendelea kubaguana baina ya Wazanzibari na Watanganyika, pia si wakati wa kuhoji nani ananufaika zaidi na kwa nini, ila kwa upeo wetu tunaamini huu ni wakati wa kushikamana zaidi, kuvuta kwa pamoja zaidi na kurekebisha kasoro zilizopo hata kama ni za kisheria ili kujenga Muungano imara zaidi. Tujitahidi kutibu kuliko kuendelea kubomoa.