Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Marubani nchini wahofia ajira EAC

25th June 2012
Print
Comments
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

Marubani nchini wameonyesha wasiwasi kuhusu kupata ajira katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa zinatolewa kwa Wakenya na Waganda tu.

Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE jana, mmoja wa wanachama wa Chama cha Marubani Tanzania (PATP) ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema ushirikiano wa kikanda  katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hautimizwi  kwa marubani wa Tanzania, bali marubani wa Kenya wamekuwa wakinufaika zaidi wakifuatiwa na Uganda.

“Pamoja na kwamba marubani wa Tanzania wanaweza kubadilisha leseni zao kuwa za Kenya, Idara ya Uhamiaji nchini humo inayohusika na utoaji wa vibali vya kazi imekuwa ikiwaeleza marubani waende kwenye Chama cha Marubani nchini Kenya (KALPA) kwa ajili ya uthibitisho wa kupewa leseni, lakini chama hicho kimekuwa kikipinga marubani wa Tanzania,” alisema.

Aidha, alisema suala hilo lilipelekwa kwa balozi wa Tanzania nchini Kenya na Mamlaka ya Usalama wa Anga Tanzania (TCAA), lakini hakuna chochote kilichofanyika hadi sasa, na kuongeza: “Tumevamiwa na marubani wengi wa kutoka Kenya kiasi kwamba wazawa hatuwezi kupata ajira.”

Alimuomba Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kuingilia kati suala hilo kwani PATP inataka kudhibiti kabisa utitiri wa marubani wa  kigeni nchini kwa kushiriki katika mchakato wa utoaji vibali kama wanavyofanya KALPA.

Alisema amefurahishwa na kitendo cha  Wizara ya Kazi na Ajira kusitisha zoezi la utoaji wa vibali vya kazi kwa marubani wa kigeni, ambapo awali (TCAA) walipeleka ombi kwa wizara hiyo na ofisi za Uhamiaji, ili kupatiwa marubani kutoka nje, kwa madai kuwa kuna ukosefu wa marubani wa ndani.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Fadhili Manongi, alikanusha madai hayo kwa kusema: “Mamlaka haiwajibiki katika ajira za marubani bali hutoa leseni tu. Kuhusu kuhusu ombi la kupatiwa marubani kutoka nje, mamlaka haijawahi kupeleka ombi hilo Wizara ya Kazi wala Uhamiaji,".


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment