Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Dau la makocha laichanganya Yanga

26th June 2012
Print
Comments
Timu ya Yanga

Uongozi  wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga ya jijini Dar es Salaam umesema kuwa zoezi la kumpata mrithi wa kocha aliyetangulia, Mserbia Kostadin Papic linakwenda taratibu kutokana na dau kubwa la mishahara ambayo makocha wanaowapendekeza wamekuwa wakitaja, imefahamika.

Hata hivyo, uongozi huo umekataa kutaja majina ya makocha wanne waliosalia katika kinyang'anyiro hicho ila wamethibitisha kwamba kwamba wanatoka nje ya nchi.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili, Abdallah Binkleb, alisema kuwa wanajipanga kufanya maamuzi sahihi na hawataki kukurupuka tena katika kuajiri kocha mpya ambaye atakiongoza kikosi chao.

Binkleb alisema kuwa hawataki kufanya maamuzi watakayojutia baadaye na vile vile wanataka kupata kocha ambaye ataipa Yanga mafanikio katika msimu ujao wa ligi.

"Kabla ya kuamua tunaangalia mambo mengi, kubwa likiwa ni gharama zake na uzoefu alionao... safari hii hatutaki kutimua tena kocha ndani ya muda mfupi," alisema Binkleb.

Aliongeza kuwa wanataka kupata kocha mwenye wasifu mzuri na ambaye atakainua kiwango cha wachezaji wao na kufanya vizuri kwenye msimu ujao.

"Tunataka kuwa na kocha ambaye ataipa Yanga mafanikio na tuwe na uvumilivu kwa kuangalia kazi na si kumtimua kama ilivyofanyika kwa makocha waliopita," Binkleb aliongeza.

Alisema kwamba hivi sasa bado wanamuamini Fred Minziro kuwa atakisimamia vyema kikosi chao licha ya mashindano ya Kombe la Kagame kukaribia.

Aliongeza kuwa ubora wa wachezaji waliowasajili unawafanya wajiamini kwamba msimu ujao, Yanga itakuwa na matokeo mazuri kwa sababu kila aliyejiunga na timu hiyo ana kiu ya mafanikio.

Yanga imeshasajili nyota kadhaa wakiwemo Ally Mustafa 'Barthez' na Kelvin Yondani kutoka Simba, Frank Domayo (JKT Ruvu), Juma Abdul, Saidi Bahanuzi (Mtibwa Sugar), Ladslaus Mbogo (Toto African) na Simon Msuva wa Moro United.

Yanga itacheza mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 14 hadi 29 hapa nchini.

Mbali na Yanga, timu nyingine kutoka Tanzania Bara zitakazoshiriki michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ni Simba na Azam za Dar es Salaam.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment