Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

‘Vijeba’ wasipewe nafasi Copa Coca Cola 2012

25th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Julai mwaka 2010, timu ya taifa ya soka ya Ghana ilitolewa kishujaa katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini.

Walipambana kwa dakika 120 na baada ya matokeo kuwa sare ya 1-1, ndipo zikapigwa penati na wao wakalala kwa mabao 4-2 katika mechi yao ya kusisimua ya robo fainali dhidi ya Uruguay.

Ghana walibaki peke yao baada ya wawakilishi wengine watano wa Afrika kuondolewa mapema; ambao ni wenyeji Afrika Kusini, Algeria, Cameroon, Nigeria na Ivory Coast.

Ingawa waliishia robo fainali, Ghana waliacha kumbukumbu nzuri katika michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Afrika kutokana na soka lao la kuvutia na kucheza kwa jihadi katika kila mechi.

Kubwa zaidi, Ghana walipendwa kutokana na ukweli kwamba kikosi chao kiliundwa na yosso wa wastani wa miaka 20. Andre Dede Ayew, Inkoum, Dominic Adiyah na Kevin-Prince Boateng ni miongoni mwa chipukizi waliounda kikosi chao cha kwanza na kuonyesha kiwango cha juu cha soka.

Si nia yetu kukumbushia tena machungu ya kuondolewa kwa timu za Afrika katika michuano Kombe la Dunia. Lakini tunaona kuna haja ya kuwakumbusha wadau wa soka nchini, hasa Shirikisho la Soka (TFF), kwamba waongeze umakini katika kusimamia michuano ya soka la vijana ili siku moja kufikia pale walipo Waghana.

Tunatambua vilevile kwamba hivi sasa, michuano muhimu ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 ya ‘Copa Coca Cola’ inaendelea kushika kasi ambapo fainali mikoa 28 inachuana huku washindi wakitarajiwa kupata kikombe na fedha taslim Sh. Milioni 8.

Michuano hiyo hufanyika kila mwaka na hakuna asiyetambua mchango wake kwa maendeleo ya soka kwani husaidia kuibua nyota wapya kwa ajili ya klabu mbalimbali za soka na pia timu za taifa.

Jambo la msingi ambalo wadau wa soka wanapaswa kukumbuka ni kwamba michuano ya Copa Coca Cola hudhaminiwa kwa fedha nyingi. Hivyo, hatua za ziada zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya vitendo vyovyote vile vitakavyoashiria ubabaishaji.

Tabia ya baadhi ya timu za mikoa kuchezesha vijana wenye umri mkubwa kuliko miaka 17 inayoruhusiwa ni miongoni mwa kero zilizowahi kuripotiwa katika miaka ya nyuma.

Kumewahi kuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusiana na ubabaishaji huu wa UMRI na baadhi ya mikoa iliwahi kukutwa na hatia ya kuchezesha vijeba wenye umri wa kucheza ligi kuu kokote kule duniani, wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 20 badala ya umri halali wa chini ya miaka 17.

Inakumbukwa kwa mfano kuwa, timu ya mkoa wa Tanga iliwahi kuondolewa baada ya kubainika kuwa ilichezesha ‘vijeba’.

Kwa kutumia faida ya kukomaa kiumri, ‘vijeba’ huonekana wazuri uwanjani kuliko yosso wa ukweli na matokeo yake, vijana sahihi huachwa na ‘vijeba’ kujazwa katika timu za taifa.

Sisi tunaona kwamba wadau wote wa soka, wakiongozwa na TFF, wanalazimika kufanya kila wawezalo kuzuia udanganyifu wa umri na kwa kuanzia, viongozi wa soka katika kila mkoa watambue kuwa udanganyifu wowote ule haifai.

Vinginevyo, ‘vijeba’ wakiachwa watawakatisha tamaa vijana sahihi wenye vipaji na pengine kutwaa ubingwa wa hila; wataondoa msisimko wa michuano ya vijana kwa sababu mashabiki wengi huwatambua ‘vijeba’ hata kwa macho. Na hatari kubwa zaidi ni kwamba wadhamini wanaweza kukatishwa tamaa na madhara yake yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Tunajua kuwa tayari kuna hatua kadhaa zimechukuliwa kukomesha vitendo vya aina hii.

Hata hivyo, tunaishauri TFF kuwa iendelee kubuni mbinu nyingine mbalimbali ili kuhakikisha kuwa michuano yote ya vijana inawashirikisha wachezaji wa umri sahihi.

Ikiwezekana, badala ya kujiridhisha na taarifa za nakala za vyeti vya kuzaliwa pekee, TFF ifanye uchunguzi pia katika vyeti halisi na vilevile, isake taarifa zaidi kutoka katika shule walizosoma washiriki.



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment