Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tumlinde Rais, asigeuzwe `mdoli` wa kisiasa

27th May 2012
Print
Comments

Sikumbuki siku, mwezi wala mwaka, lakini wakati akiwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliwahi kushiriki harambee ya kuchangia Kanisa Katoliki lililopo maeneo ya Mbezi Tanki Bovu jijini Dar es Salaam.

Kabla ya harambee hiyo, kulikuwa na Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo. Mimi pia nilihudhuria.

Moja ya jambo lililojiri wakati wa harambee ile, ni kitendo cha muongozaji wa shughuli ya harambee, kujata mara kwa mara wadhifa na jina la Waziri Mkuu, Lowassa.

Ilikuwa ni hekaya za “Waziri MKuu atafanya hivi, Waziri Mkuu atafanya vile…” akarudia mara kwa mara hata kufikia hatua ya kusema “toeni michango mingi ili muone Waziri Mkuu Lowassa atakavyoonyesha uheshimiwa wake.”

Ilivyoonekana ni kama Lowassa alikuwa anamvumilia muongoza shughuli ya uchangiaji, pengine kwa vile Kardinali Pengo alikuwepo. Si kwamba alimuogopa, bali kwa heshima na kutekeleza misingi ya itifaki.

Lakini akiwa katika kuchangisha fedha, tena kwa kuwataja watu kwa majina yao, muongoza harambee aliendelea na ‘vibweka’ vyake, ndipo Lowassa akafungua kinywa na kumuonya.

Maneno ninayoyakumbuka alisema “ MC naomba usiendelee kutaja cheo na jina la Waziri Mkuu kimzaha, hapa tupo kazini ukiendelea nitaomba wakusimamishe.”

Kuanzia hapo muongoza harambee akafyata mkia, hakutaja wadhifa wala jina la Waziri Mkuu Lowassa kwa mzaha. Akakoma, akaheshimu.

 

Si Kardinali Pengo aliyeonyesha kukerwa na tamko la Lowassa, si Paroko wa parokia ile, Katekista, Mwenyekiti wa Walei ama mwanachama wa Utoto Mtakatifu, aliyeonyesha kukerwa na agizo la Lowassa. Lilistahili.

Fundisho lililokuwepo mahali pale ni kwamba, akiwa katika mamlaka za watu (kidunia), Waziri Mkuu ni mtu wa kuheshimika sana. Hivyo binafsi anastahili kujiheshimu ili jamii imheshimu.

Lakini hata pale ‘anapochezewa’ kwa kejeli na dharau, tena mbele ya umma wa Watanzania, kiongozi wa umma hapaswi kucheka, hapaswi kutabasamu, hapaswi kuukubali mzaha.

Akilibaini hilo, kwamba ‘anachezewa’, anafanyiwa kejeli na dharau mbele ya umma wa Watanzania, basi anajenga na kupanua wigo mpana wa ‘kuzewa’, kufanyiwa kejeli na kudharauliwa mbele ya umma. Hadhi na mamlaka za kimaadili zinaathirika.

Ninalisema hilo kwa sababu, hivi karibuni, Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda, alikaririwa ‘akimchezea’ na kumkejeli Rais Jakaya Kikwete.

Akiwa katikati ya kundi na viongozi wakiwemo waandamizi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Rais Kikwete, Shibuda akatangaza nia ya kugombea Urais mwaka 2015.

Sina shaka na nia hiyo, ingawa imezua malumbano yasiyo na msingi ndani ya chama chake. Lakini hoja yangu leo ni kauli yake dhidi ya Rais Kikwete.

Kwamba atakapotimiza azma yake kuwania urais 2015, atamteua Rais Kikwete kuwa Meneja wa kampeni zake. Ni kumchezea Rais, ni kumkejeli Rais. Haipaswi kufanyika wakati wowote wa majira ya siku.

Iwe alfajiri, asubuhi, mchana, alasiri, adhuhuri, jioni ama usiku. Haipaswi itokee kauli si tu kama alivyotamka Shibuda, bali hata kuwa na mwelekeo ama dalili na ishara za kauli kama hiyo.

Kufanya hivyo si udikteta, kufanya hivyo si ukiukwaji wa haki za binadamu, kufanya hivyo jambo jingine zaidi ya kulinda hadhi ya urais nchini.

Kumkabidhi Rais wa nchi jukumu la kuwa Meneja wa kampeni wakati akiwa bado yupo madarakani ni fedheha kubwa kwa Watanzania. Haikustahili na haistahili kufanyika hata kwa sekunde moja iliyo ndani ya siku 365 za mwaka.

Katika hali ya kustaajabisha, hakuna kiongozi aliyekerwa na tamko la Shibuda, hakuna kiongozi alikemea tamko la Shibuda, hakuna, hakuna kiongozi aliyepinga tamko la Shibuda.

Ni kama waliokuwepo walilipokea tamko la Shibuda wakicheka, wakifurahi, wakilipongeza,wakilikubali, wasiijue wala kuitambua thamani ya Urais katika mamlaka za watu.

Kumchezea Rais wa nchi ni kuuchezea umma, kumkejeli Rais wa nchi ni kuukejeli umma, kumdhalilisha Rais wa nchi ni kuudhalilisha umma.

Itakuwaje kwa Rais Kikwete ambaye ifikapo 2015, hata wakati wa kampeni za urais zitakapofanyika, atakuwa anaendelea kwa wadhifa huo, akabidhiwe jukumu la Umeja wa kampeni, tena kwa mgombea anayejitangaza hata nje ya utaratibu wa chama chake?

Rais anapohusishwa kwenye tukio lenye taswira ya kejeli, likifanyika kwa kejeli tena kinyume cha utaratibu, kinachostahili kufuata ni kukemea, kuonya na kukaripia.

Mshereheshaji wa harambee ya kuchangia Kanisa Katoliki kule Mbezi Tanki Bovu alipoendelea kutaja wadhifa na jina la Waziri Mkuu Edward Lowassa kwa kejeli, alikemea, akanyamazishwa. Ilikuwa kulinda heshima na hadhi ya Waziri Mkuu.

Viongozi wa CCM waliokuwepo wakati Shibuda akitoa tamko hilo walishindwa vipi kumdhibiti, kumkemea na kumkaripia?

Wameonyesha wazi kwamba hawakuliweza hilo. Hivyo jukumu hili libaki kuwa mikononi mwa umma. Rais wa nchi asigeuzwe kuwa mfano wa mdoli wa kisiasa wa `kuchezewa’ na mtu yeyote na mahali popote. Haistahili.

Kejeli zinazopoanza kwa mtindo huo dhidi ya Rais wa nchi, zikaachwa ziendelee taratibu, hatua kwa hatua, hadhi yake inashuka na atazidi kuchezewa.

Rais wa nchi alindwe, Rais wa nchi asifanyiwe kejeli na mizaha ya ‘kitoto’, Rais wa nchi aheshimiwe. Kwa kufanya hivyo, mambo yanayompasa Rais wa nchi yatakuwa yenye maslahi na uzito unaostahili.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540, 0716635612 au barua pepe; mgeta2000@yahoo.com

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment