


Mhariri wa Kampuni ya New Habari Cooperation, Martinyi Masyaga (41) mkazi wa Jiji Dar ss Salaam, na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya hakimu Mkazi Arusha, kujibu shitaka la kuomba nakupokea rushwa ya sh milioni 1.5.
Akisoma hati ya mashitaka, Mwendesha mashitaka, Hamidu Simbano, akisaidiana na Rehema Mteta, mbele ya hakimu Yohana Myombo, alidai kuwa washitakiwa kwa pamoja mnamo Juni 13 na 14, mwaka huu, majira yasaa 10.00 jioni wilayani Monduli kwa pamoja waliomba rushwa ya sh milioni 1.5 toka kwa Afisa wa Tanesco wa Wilaya hiyo, Andrew Mahamdu.
Alidai kuwa rushwa hiyo ilikuwa na lengo la kumshawishi ili wasimwandike gazetini, kama alikuwa mwajiriwa asiyestahili kuwepo katika nafasi hiyo.
Mwendesha mashitaka huyo aliendelea kusoma shitaka la pili, ambalo lilimuhusu mshitakiwa wa pili, Mwita Chomete (32), ambaye ni mfanyakazi wa mifumo ya kompyuta ofisi za New Habari Cooperation, mkazi wa Dar es Salaam, anadaiwa siku hiyo ya tukio, alipokea sh. 200,000 toka kwa mfanyakazi wa Tanesco, Andrew Mahamdu, kwa niaba ya Masyaga.
Mshitakiwa wa tatu katika shitaka hilo alitajwa kuwa ni Bora Bidiga (36), mkazi wa Jiji Arusha, ambaye mara baada ya kudhaminiwa alipotea mahakamani hapo na ndugu zake.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo washitakiwa walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana ya masharti ya kudhaminiwa mdhamini mmoja anayejulikana na kampuni iliyosajiliwa ya jijini Arusha na kusaini bondi ya sh. 500,000.
Washitakiwa wote walidhaminiwa, ambapo Martinyi Masyaga alidhaminiwa na Felix Mohamedy (48), mkazi wa Unga Limited jijini Arusha na kesi imeahirishwa hadi Juni 29, mwaka huu itakapotajwa tena.