Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Sumatra, Polisi wabuni mbinu mpya kuwashughulikia madereva wa daladala

15th June 2012
Print
Comments
Mkurugenzi wa Sumatra, Kitengo cha Udhibiti Usafiri wa Barabara, Aron Kisaka

Mamlaka  ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu  na Majini (Sumatra) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, imebuni mbinu mpya ya kuwashughulikia madereva wa daladala wanaovunja sheria ambapo tayari 11 wameshatiwa mbaroni.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Sumatra, Kitengo cha Udhibiti Usafiri wa Barabara, Aron Kisaka, alisema mbinu hiyo inahusisha  kuwakamata madereva hao na kuwasweka rumande na kisha kuwapandisha kizimbani.

Alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya mamlaka hiyo na polisi, kilichofanyika wiki iliyopita, ambapo mambo matatu yalijadiliwa.

Aliyataja mambo hayo kuwa  ni kubuni mbinu mpya ya kuwashughulikia madereva hao,  kuangalia makosa yatakayopewa uzito ikiwa ni pamoja na kuzidisha nauli, kuiba safari na kukatisha safari; na aina ya adhabu iatakayotumika.

Kisaka, aliongeza kuwa, utekelezwaji wa mbinu hiyo ulianza mara moja baada ya kikao hicho, ambapo madereva 11 wa daladala zinazofanya safari zake kati ya Mwenge na Posta, Posta na Mwananyamala, na Mwenge kwenda maeneo mengine  wamekamatwa na kuswekwa rumande na jana walifikishwa mahakamani.

Uamuzi huo umekuja baada ya hivi karibuni Sumatra kutangaza operesheni ya kuwafutia leseni wamiliki na madereva wa daladala na pikipiki ambao watapatikana na makosa ya upandishwaji nauli kiholela, ukatishwaji safari na kuiba safari.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment