Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Uongozi soka la Bongo unahitaji sura mpya

23rd June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Shirikisho la soka (TFF) linataraji kufanya uchaguzi wake mkuu mwingine mwisho wa mwaka kwa ajili ya kuchagua rais na kamati yake ya utendaji.

Tayari kamati ya uchaguzi ya TFF imetoa ratiba ya uchaguzi huo ambapo vyama wanachama wa shirikisho hilo vimetakiwa kufanya chaguzi zake kati ya Julai 1 na Novemba 10.

Kimsingi tarehe hizo na chaguzi hizo za ngazi mbili ni mpya lakini kutokana na taarifa za uhakika ambazo Nipashe tunazo, chaguzi zote hizo hazitatoa viongozi wapya kwa maana halisi ya upya.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba chaguzi hizi zinatarajiwa kuhusisha nyingi ya sura zile zile ambazo kwa miaka mingi ya mchezo huo nchini zimekuwa ama kwenye madaraka ama karibu na madaraka hayo na pasiwe na maendeleo yoyote katika soka letu.

Ni kweli tumeshuhudia utulivu katika uongozi wa TFF tangu kubadilika kwa shirikisho hilo kutoka kilichokuwa chama (FAT) lakini maendeleo pekee ambayo yanaonekana wazi ni amani na utulivu, basi.

Maendeleo pekee ambayo yameonekana ni amani na utulivu katika ofisi za shirisho, nje ya uwanja, kwa sababu kimsingi wengi wa viongozi walioshika madaraka tangu mwaka 2004 ni wale wale waliokuwa karibu na madaraka ya soka kwa kipindi chote cha uhai wa mwishoni wa FAT.

Nafasi ya timu ya taifa, Taifa Stars, katika chati za FIFA, shirikisho la soka la dunia, kwa mfano, imekuwa ikiongezeka ukubwa wa namba kwa kasi tangu mwaka huo wa 2004.

Ni vigumu kuamini, kwa mfano pia, kwamba nchi haina tena madaraja ya asili ya soka ambayo yana umuhimu mkubwa katika kuhakikisha maendeleo ya mchezo huo kote nchini kutokana na kushirikisha si tu wachezaji wengi kwa mara moja bali pia wachezaji wengi kwa muda mwingi wa msimu mmoja.

Ni vigumu kuamini nchi imebaki na utitiri wa timu zinazocheza mechi mbili-tatu za ligi za wilaya kabla ya wachezaji kutawanyika na vipaji kupotea.

Ni vigumu kuamini nchi imebaki na ligi iliyojaa timu za majeshi zinazomudu kuwa na nafasi ya kuonekana kuwa na uwezo wa kupanga matokeo katika kila ngazi ya ligi za TFF.

Lakini pamoja na mapungufu haya ambayo ni sehemu ndogo tu ya udhaifu wa TFF hatutashangaa, kama chaguzi za Julai mosi mpaka Novemba 10 zitarudisha msingi ule ule mbovu uliojengewa 'nyumba' kwa miaka nane iliyopita.

Sababu ni kwamba Julai mosi si mbali, na kwa mantiki hiyo tunachukua fursa hii kuomba wajumbe wa mikutano mikuu ya uchaguzi ya mikoa ambayo haijafanya chaguzi zake mpaka sasa kujitahidi kufanya maamuzi kwa kuzingatia kipya ambacho mgombea anaweza kuupa, kwanza, mkoa na baadaye mkutano mkuu wa TFF.

Wajumbe kutoka wilayani waache mazoea ya kuchagua viongozi wa mikoa kwa kutumia kigezo cha majina yaliyozoeleka ili kubomoa msingi wa mwaka 2004 na 2008 ambao umelifikisha taifa hapa lilipo licha ya bahati kubwa ya kuwa na Rais JK mwenye mapenzi makubwa katika michezo na hasa soka.

Ni msingi ambao umelifikisha taifa hapa lilipo licha ya ushawishi wa Rais JK kuvutia wadhamini kujitokeza kwa nguvu kubwa kuliko ambavyo iliwahi kutokea katika miaka 50 ya uhuru wa nchi katika kudhamini Taifa Stars.

Ni msingi ambao umetupa viongozi wa TFF ambao hawako tayari kuzisadia klabu kuwa na hali njema kiuchumi kwa kupunguza makato yatokanayo na mapato ya milangoni licha ya shirikisho, tofauti na FAT, kuwa na vyanzo kadha mbadala vya mamia ya mamilioni ya shilingi yahusikayo na udhamini wa ligi kuu ama Taifa Stars.

Ni msingi ambao umetupa viongozi wa TFF ambao hawako tayari kuachia ligi kuu ya Bara iendeshwe na kampuni kwa lengo la kuvutia wadhamini wa-ukweli ambao moja ya masharti yao ya msingi ni kuwepo kwa shindano huru nje ya shirikisho la soka.




SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment