Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tukatae biashara ya wahamiaji haramu

3rd July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Ni hakika kuwa wimbi la wahamiaji haramu ambao ama wanaingia nchini kwa nia ya kupita kuelekea kwingineko au pengine kupata makazi ni kubwa. Juni 26, mwaka huu maiti 43 raia wa Ethiopia, ziliokotwa kichakani katika kijiji cha Chitego, wilayani Kongwa, Dodoma, pia walipatikana watu 84 wakiwa hai, lakini wote wakiwa wamedhoofu sana kiasi cha kukaribia kufa kutokana na kukosa chakula na maji kwa muda mrefu.

Habari kutoka kwa walionusurika kifo zinasema kuwa Wahabeshi hao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. 

Inadaiwa kuwa safari yao ilianza miezi mitano iliyopita.  Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi.  Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa kukosa hewa.

Tukio la wahamiaji haramu lililoripotiwa Dodoma siyo la kwanza kutokea hapa nchini, taarifa za kiusalama zinasema kuwa katika kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia nchini. 

Mathalan, kati ya mwaka 2005 na Juni mwaka huu wahamiaji haramu 19,683 wamekwisha kukamatwa, asilimia kubwa ya kundi hilo wamekwisha kuondoshwa nchini, ingawa kiasi cha watu 1,500 wako  magerezani wakitumikia vifungo na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi kati yao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na Bangladesh.

Mbali na tukio la Dodoma, kumbukumbu zinaonyesha kuwa wahamiaji haramu 21 walikufa Desemba mwaka jana mkoani Morogoro, huku kukiwa na wengine 12 waliokufa katika matukio mawili ya mkoani Mbeya, Mei mwaka huu.

Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kupitia njia zisizo rasmi, njia kuu ni maeneo ya mipakani ya mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa nchi kavu, pia wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara kama Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.

Ingawa ardhi ya Tanzania inatumika katika biashara hiyo haramu, madhumuni yao siyo kuishi nchini ila kupitia njia kwenda Afrika Kusini ambako wanafanyiwa mipango ya kwenda kuishi Marekani na nchi za mataifa ya Ulaya; kwa maneno mengine Tanzania ni njia ya kupita, lakini hawapiti hivi hivi tu, wanalipa fedha.

Matukio haya yanayojirudia rudia nchini kwa vifo vingi vya wahamiaji haramu vinaweka hadharani siri kubwa kwamba kuna watu wanafanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, tena wanaifanya ndani ya mipaka ya nchi hii kwa kutumia usafiri duni sana wa malori kama mizigo tena yakiwa yamezibwa kiasi cha kuwakosesha hewa na hivyo kufa.

Usafisishaji wa binadamu ni biashara haramu kwa mujibu wa sheria za nchi hii na hata zile za kimataifa; kwa maana hiyo wanaoifanya wanajua wazi kuwa wanavunja sheria. Tunafikiri siyo haki watu hawa wenye tamaa ya fedha hata kwa kuuza binadamu wenzao kuitumia ardhi ya taifa hili kuendesha unyama wao dhidi ya ubinadamu.

Tumemsikia Rais Jakaya Kikwete akisema wazi kuwa ameagiza vyombo vya usalama kujipanga sawa sawa katika kukabiliana na wimbi la biashara hii haramu, lakini pia amefanya mawasiliano na wakuu wa nchi ambako biashara hii inafanyika, kwa maana hiyo, Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini ili  kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria, nia ikiwa kudhibiti mtandao huo ambao unaonekana kuota mizizi katika eneo hili la Afrika.

Pamoja na juhudi hizo za serikali, tunaamini kuwa mikoa ya mipakani ya kaskazini kwa maana ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kuna mtandao ambao umejiimarisha katika biashara hiyo ndiyo maana husikii wahamiaji haramu wakikamatwa huko, ila hukamatwa wakiwa katikati kabisa ya nchi.

Swali la kujiuliza hapa ni je, ndani ya mikoa hiyo hakuna vyombo vya usalama vinavyofanya kazi zake sawasawa?

Tunajiuliza swali hili kwa sababu wahenga walituasa ‘mvunja nchi ni mwananchi’ kwa maana hiyo kuna hisia kwamba vyombo vya usalama katika maeneo haya vinaweza kuwa vimefumbia macho biashara hii au tuseme tu baadhi ya wahusika katika vyombo vivyo wananufaika nayo.

Ni kwa maana hiyo tunapendekeza kuwa macho ya serikali yaelekezwe zaidi kwenye chanzo na kuwawajibisha watendaji wetu katika maeneo hayo.

Wahamiaji haramu ni watu hatari kwa usalama na ustawi wa taifa, kwa mtindo huo, siyo ajabu kujikuta kuwa tamaa ya fedha inasababisha hata kuvisaidia vikundi vya kigaidi na matokeo yake umma ndio utaumia.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment