Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Amenitolea mahari, ni mjamzito lakini mchumba huyu ananikataa…nifanyeje?

17th June 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita tumeona vijana wanavyopata misukosuko wakati wa kusaka wachumba. Mwingine anasema japo hajamposa anamlazimisha amtumie fedha mara kwa mara.

Mwingine anawaahidi wachumba zaidi ya mmoja kuwa atawaoa, jambo ambalo baadaye linampa mtihani amuoe yupi na kadhalika.

Wapo baadhi ya wasomaji baada ya kuisoma makala ile wametoa visa vinavyowahusu ambavyo vinakaribia kufanana na vya wenzao.

Kwa mfano wiki iliyopita yupo kijana aliyesema kuwa ana wachumba wawili na kila mmoja anajua ataolewa naye, lakini pia kabla ya kuwa na wachumba hawa, ana mtoto aliyezaa na mwanadada mwingine.

Kijana huyu nilimshauri kwamba kama kwa kuwa na wachumba hao kwa mpigo huku wote kila mmoja kwa wakati wake bila kujijua yupo mpinzani, akiamimi kuwa ndiye atakayeolewa kunamkwaza, basi ni afadhali achukue maamuzi magumu ya kuwatosa wachumba hao na kumuegemea yule aliyezaa naye mtoto kama bado angali anampenda. Kwa hao wachumba wawili alitakiwa kuachana na mmoja wao mapema na siyo wote kuwapa matumaini.

Baada ya kisa cha kijana huyu kuchapishwa gazeti la NIPASHE Jumapili iliyopita, yupo binti mmoja aliyetuma ujumbe wake akisimulia kisa kilichomsibu ambacho anakifananisha na hicho alichokisoma.

Anasema; Anti mimi naitwa Jose(siyo jina halisi), nina kijana mchumba wangu ambaye tayari ameshanitolea mahari. Lakini cha ajabu ni kwamba amekuwa ananitamkia kuwa hatanioa tena kwani ameamua akamuoe mwanamke mwingine ambaye alishazaa naye. Nifanyeje?”

Nami nikamshauri hivi kwamba; maadam amemtamkia hivyo huku akijua kuwa ameshapeleka mahari, basi bibie amwambie kitaitishwa kikao cha familia pande zote mbili kama zilivyokutana wakati wa kutoa na kupokea mahari, kisha kijana huyo aseme maneno hayo mbele za mashahidi hao, kisha jambo hilo lijadiliwe.

Wakati nikitoa ushauri huo, bibie huyu akaniambia; “ isitoshe anti mimi tayari ni mjamzito nina mimba yake”. Nikamuuliza; Je, anajua kuwa wewe ni mjamzito? Akanijibu; “anajua na ajabu ameniambia niitoe hii mimba kwa sababu hatanioa na kwamba anataka kuishi ya yule mwanamke aliyezaa naye waweze kutunza mtoto wao.

Nikamuuliza tena, je, huyo kijana unaishi naye au yuko kwake? Akajibu; anaishi kwangu na wazazi wake wananipenda kwani wananiambia nikimuacha kijana wao atakufa.

Lakini cha ajabu hata jana nimekuta eneo la kitanda limechorwachorwa na nimeshakuta madawa ya kiganga kwani huyo mwanamke wake ni mshirikina sana ila mimi ni mtu wa maombi Mungu wangu ananipigania.

Mpenzi msomaji, alivyotamka yote hayo nikagundua kwamba nguvu za giza ndizo zinazomuumiza kijana huyo na siyo ajabu hajitambui bali anapelekeshwa tu na huyo mzazi mwenzake.

Kijana huyu kwa hiari yake alikubali kwenda kumtolea mahari bibie huyu na hatua hiyo aliichukua huku akiwa tayari alishazaa na mwanamke mwingine.

Nimejiuliza maswali kadhaa kwamba kama alikuwa bado anampenda mwanamke huyo aliyezaa naye kwanini hakwenda kumtolea mahari?

Na kwanini hata wazazi wa kijana wanampenda huyu anayekataliwa na siyo huyo mwenye mtoto tayari? Mpenzi msomaji, kila nilipotafakari mtafaruku huu, jibu linalonijia ni kwamba mapepo yanamsumbua kijana huyo. Kama huyo mwanamama aliyezaa naye anategemea nguvu za giza(ushirikina) ili kijana huyo amuoe badala ya huyu aliyemtolea mahari naambaye pia tayari naye ni mjamzito, mahusiano hayo hayatadumu.

Hayo ni majaribu ya shetani ambayo kwa sasa hayana nafasi kwa wale wamtegemeao Mwenyezi Mungu. Hawa watapambana lakini hawatashinda, maneno ya Mungu yanasema. Alichonifurahisha bibie huyu ni pale aliposema kuwa haogopi madawa yanayoingizwa ndani mwake kwa kuwa mkono wa Mungu una nguvu atayateketeza.

Mpenzi msomaji, wapo watu katika ulimwengu huu ambao kazi yao ni kubomoa ngome za wenzao na wakishafanikiwa wanakaa kando wakichekelea. Hawa ni mapepo na kwa jina zito ni mashetani.

Wanaume wamekuwa wepesi kupumbazwa na nguvu za kishirikina kutokana na ukweli kwamba vinara na ambao utawakuta kwa wingi kwa waganga wa kienyeji ni wanawake. Kule wengine wanatafuta kufarakanisha ndoa za wenzao.

Wengine wanataka vyeo vya wenzao yaani wanawapiga dhoruba wenzao ili watimuliwe kazini au waondoshwe kwenye nafasi fulani wakae wao. Hawa wanasahau kwamba kila mtu mbele za Mwenyezi Mungu ana fungu lake kwa maana ya hazina yake kule mbinguni. Ndivyo maandiko ya Mungu yanavyotueleza.

Na kwamba kilichofunguliwa hapa duniani na binguni kimefunguliwa. Hali kadhalika kilichofungwa duniani na Mbinguni kimefungwa hivyo hakuna haja ya mtu kutapatapa. Pia mke mwema hutoka kwa Mungu. Sasa kwanini wanadamu warukeruke kuvuruga wengine?

Watu wengi wamemsahau Mungu wakitegemea zaidi wanadamu na nguvu za giza ambazo hazidumu. Haya siyo maisha na ndiyo maana hata yule aliyedhani kafanikiwa sana kutokana na ujanja ujanja, anguko lake huwa kubwa sana, tena la aibu.

Kijana tuliyemzungumzia hapo juu ambaye alishatoa mahari na sasa anamtamkia mchumba wake kuwa hatamuoa, naamini siyo mamlaka yake. Na ndio maana hata wazazi wake wanang’ang’ania binti huyo asimwache kwani ataharibikiwa kimaisha.

Binti huyu baada ya ujumbe wake kwenye simu ilibidi nimpigie. Anaonekana ni mcha Mungu mzuri na ndiyo maana majaribu yote pamoja na kuletewa madawa ndani ambayo bila shaka anapewa kijana wake huyo ayalete anayashinda.

Nikampa moyo kwamba maadam anamtegemea Mungu amwamulie, asiogope. Kwani maandiko yanasema, Mungu akiwa upande wako ni nani atakaa juu yako?

Msomaji wangu, kwa leo niishie hapa upate nawe kuchangia maoni. Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment