Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Cirkovic kuisuka upya Simba

26th June 2012
Print
Comments
Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic

Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, leo saa 10:00 jioni ataanza kukisuka upya kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa kwa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itakayofanyika  jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 14 hadi 29.

Cirkovic alirejea nchini juzi usiku akitokea kwao ambako alikwenda likizo baada ya msimu wa ligi uliopita kumalizika Mei 6 mwaka huu.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa mazoezi ya Cirkovic yataanza saa 10:00 jioni na lengo ni kujiweka tayari kwa mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kushirikisha timu zaidi ya 12 kutoka nchi mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na timu zitakazoalikwa kutoka katika maeneo mengine ya ukanda huo.

Kamwaga alisema kwamba ujio wa kocha utawasaidia kurekebisha upungufu ulioonekana katika mechi mbili za kirafiki zilizofanyika walizocheza hivi karibuni katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Kamwaga alisema kuwa kikosi chao, kikiwa Kanda ya Ziwa,  kilionyesha kiwango cha juu na wana imani kwamba watafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa na pia katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

"Kocha amesema anataka kukutana na wachezaji uwanjani kesho saa 10:00 na moja kwa moja ataendeleza mazoezi kwa sababu hata kile ambacho walikuwa wanafanya chini ya msaidizi wake (Amatre Richard) kilitokana na maelekezo yake," Kamwaga alisema.

Aliongeza kuwa mwishoni mwa wiki kocha huyo atakutana na benchi la ufundi la Simba ili kujipanga upya na kikubwa ni kuangalia namna zoezi la usajili lilivyoendeshwa.

Wakati huo huo, habari kutoka katika kamati ya ufundi ya Simba inaeleza kwamba Kamati ya Usajili imedaiwa kufanya usajili bila ya kuzingatia mapendekezo ya kocha huyo.

Chanzo kimeeleza kuwa mapendekezo ya kusajili zaidi vijana hayakufanyiwa kazi na badala yake yosso hao kutoka Simba B wameachwa na timu hiyo ya vijana iko katika hatihati ya kuvunjwa.

Juzi, mabingwa hao wa Bara walitoka sare ya 1-1 dhidi ya  Express ya Uganda ambako Kigi Makasi aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu wao, Yanga ndiye aliyewafungia Simba goli la utangulizi kabla wageni kusawazisha.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment