Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Miradi ya maji ipewe kipaumbele

10th July 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Jana Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, aliwasilisha bungeni mjini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 huku akielezea mikakati mbalimbali jinsi serikali ilivyojipanga kutatua tatizo la maji nchini.

 Waziri Maghembe aliliomba Bunge liidhinishe Sh. bilioni 485.8 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huo wa fedha.

Kama tunavyojua maji ni uhai na ni muhimu kwa maisha ya binadamu, mifugo, mimea na hata wanyama wa porini.

Ni kwa msingi huo, ndiyo maana baadhi ya wabunge baada ya Waziri Maghembe kuwasilisha bungeni hotuba yake hiyo ya makadirio na mapato kwa mwaka ujao wa fedha, walilazimika kuibana serikali wakiitaka ieleze sababu za miradi yake mbalimbali ya maji, ukiwamo ule unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) wa kupeleka huduma hiyo kwenye vijiji 10 katika kila halmashauri nchini ulioahidiwa kwa zaidi ya miaka sita iliyopita bila kutekelezwa.

Katika hatua hiyo, baadhi ya wabunge, wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walitishia kutounga mkono bajeti ya Wizara ya Maji iwapo hawatapata majibu ya kuridhisha kutoka serikalini juu ya hatima ya miradi hiyo ya maji.

Miongoni mwa wabunge walioibana serikali kuhusu kutotekelezwa kwa mradi wa maji unaofadhiliwa na WB, ni Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM), ambaye alisema mradi huo umekuwa ukisuasua sana kana kwamba, kuna mganga wa kienyeji katika kuutekeleza.

Aidha, Mbunge mwingine alidiriki kusema kama isipoangaliwa kwa umakini, Vita Vikuu vya Dunia vya Tatu, vyaweza kusababishwa na tatizo la maji.

Kwa ujumla, wapo wabunge waliowalaumu wabunge wenzao ambao wanalalamika kwamba kwenye majimbo yao hakuna maji lakini jambo la kushangaza wanaunga mkono hotuba ya bajeti.

Kauli kali kama hizi za wabunge zinatokana na umuhimu mkubwa wa maji kwa maisha yote ya binadamu.

Baadhi waliishauri serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba maji yatokanayo na mvua yanavunwa pamoja na kutunza mazingira na vyanzo vya maji kwa gharama zozote zile.

Kimsingi, karibu kila mbunge aliyeinuka kuchangia hotuba ya Waziri Profesa Maghembe, alielezea tatizo kubwa la maji jimboni kwake na kuzilalakimikia mamlaka za maji katika halmashauri zao kuwadai wananchi kulipa bili pasipo kuzingatia huduma itolewayo.

Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, alisema tangu aingie bungeni miaka minane iliyopita, serikali imekuwa ikiahidi kupeleka maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma kupitia miradi inayofadhiliwa na mashirika mbalimbali, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Lakini alishangazwa kwamba wakati Manispaa ya Kigoma wakikosa maji, wamekuwa wakipandishiwa malipo ya ankara za huduma hiyo huku kila mtumiaji wa maji akitakiwa kulipa sawa na mwingine bila kujali tofauti ya muda wa matumizi ya kila mmoja.

“Mimi leo sitaunga mkono hoja (bajeti) ya (Wizara ya) Maji mpaka niambiwe hizi ankara za maji kwanini watu wasitozwe kulingana na wanavyotumia? Mimi sina shida na kupandisha bei ya maji, Lakini tutozwe kulingana na tunavyotumia,” alisema Serukamba.

Aliongeza: “Anayetumia maji mengi alipe pesa nyingi. Haiwezekani mtu wa Ujiji kule anapata maji mara moja unamtoza sawa na mtu wa Mji Mwema anayepata maji mara tano."

Ndivyo ilivyo hata katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ni jambo la kawaida kwa wateja kusuguana na mamlaka husika za maji kuhusiana na tatizo hilo kama ilivyo kwa majiji na halmashauri nyingine hapa nchini.

Ukosefu wa maji umewafanya hata baadhi ya wananchi katika maeneo mengine kuchangia na mifugo hususan katika maeneo ya wafugaji.

Mbaya zaidi ni kwamba hata hayo wanayochangia na mifugo si maji safi na salama bali ni yale yaliyotuwama yakiwa na matope, viluwiluwi na kinyesi cha ng'ombe.

Ni kwa msingi huu ndipo tunapoona umuhimu wa serikali kujipanga vilivyo kuhakikisha kwamba miradi mingi ya maji inayopangwa, itekelezwe ili wananchi wanufaike na huduma hiyo muhimu.

Kwa hakika, bila maji hakuna uhai, maradhi mengi sana huibuka katika jamii chanzo chake kikubwa kikiwa ni maji.

Mbali ya maji kutumika kwa kupikia chakula, lakini pia ni nyenzo muhimu kwa usafi wa karibu kila kitu, kuanzia binadamu mwenyewe, makazi yake, mavazi yake na vyombo vyake vya majumbani.

Hii ina maana kwamba pasipo maji, hakuna usafi na hatma yake ni mlipuko wa magonjwa mbalimbali na hivyo kuchangia kudumaza uchumi wa nchi kwa kuwa hakuna taifa litakalojengwa na wananchi wagonjwa.

Ni umuhimu basi serikali pamoja na vyanzo vya maji vilivyopo sasa, ifanye juhudi ya kuvitambua vingine ili maji hayo yawafikie wananchi vijijini na mijini.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment