Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Zoezi la uokoaji lazidi kuwa gumu

22nd July 2012
Print
Comments

Wazamiaji katika ajali ya meli MV Skagit wamesema kazi ya uokoaji imekuwa ngumu kutokana na kukabiliwa na uhaba wa vifaa vya kisasa vya kusadia kufanya kazi hiyo.

Wakizungumza na NIPASHE wazamiaji hao walisema kwamba pamoja na kazi hiyo kufanyika jana baada ya kusita kwa muda bado wameshindwa kuiona mali hiyo kutokana na kuzama katika mkondo mkubwa wa bahari.

Mzamiaji Ali Ramadhan, alisema kwamba tangu kuzama kwa meli hiyo wazamiaji 10 wametumika kupiga mbizi chini ya bahari kutafuta meli hiyo bila mafanikio yoyote.

Alisema kwamba eneo ambalo waliona mafuta machafu yakisambaa kwa wingi juu ya bahari waliweka maboya kwa kutumia nanga lakini bahati mbaya jana wameshindwa kutambua eneo hilo baada ya maboya kupotea.

Ramadhan alisema kimsingi jana hawakufanikiwa kupata hata maiti moja lakini alisema kwamba uwezekano wa meli hiyo kuonekana ni mdogo.

Alisema kwamba tangu kuzama kwa meli hiyo mara ya kwanza wazamiaji wanne walipinga mbizi baharini lakini hawakufanikiwa kuona meli hiyo na wengine sita kufanya kazi kama hiyo bila ya mafanikio yoyote.

“Jambo la msingi kwa serikali kujipanga na kutafuta vifaa vya kisasa vya kukabiliana na majanga kama haya lakini uokoaji umekuwa mgumu kutokana na tatizo la ukosefu wa vifaa vya kisasa,” alisema Ramadhan.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, alisema serikali imeamua leo kufanya kisomo cha hitima ya kuwaombea marehemu waliyopoteza maisha katika ajali hiyo.

Alisema kwamba hitma hiyo itafanyika katika msikiti Mkuu wa Mwembeshauri Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na msikiti Mkuu wa Kisiwani Pemba.

Alisema kwamba hadi sasa watu 77 bado hawajapatikana ambapo watu 68 wamekufa na watu 146 waliokolewa.

Alisema kwamba hitma hiyo itafanyika baada ya sala ya adhuhuri na kuwataka wananchi kujitokeza katika ibada hiyo.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment