Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mnyika ajipanga kubadili kanuni za Bunge

25th June 2012
Print
Comments
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, ameanza mchakato wa kuwasilisha bungeni mapendekezo ya kuzifanyia marekebisho Kanuni za Kudumu za Bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga sheria kuhusiana na mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka ya 107 ili kuongeza nguvu za Bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa madaraka ya Bunge, Ibara ya 63 (2) na (3) ya Katiba ya sasa.

Kwenye taarifa yake aliyoitoa jana jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema amefikia hatua hiyo kutokana na hali iliyojitokeza hivi karibuni bungeni, ambapo Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 na Bajeti ya Mapato na Matumizi ya serikali  vilipitishwa bila ya marekebisho yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kuikosoa.

Alisema kwamba kupitishwa kwa mpango wa maendeleo na bajeti hiyo katika mazingira yalivyokuwa, kunaonyesha kudhihirika kile alichotahadharisha tangu awali kwamba mbali na udhaifu wa kikatiba wa kutoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na uendeshaji wa nchi, lakini pia udhaifu wa kanuni za kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni ya 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge haruhusiwi kupendekeza mabadiliko yoyote katika makadirio na mapato ya serikali.

“Katika mazingira haya, udhaifu wa Rais na uzembe wa Bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na serikali kutokana na ufisadi ikiwa ni pamoja na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida, lakini pia inachochea migomo baridi ya watumishi wa umma hususani madaktari, walimu na askari kutokana na madai yao ya muda mrefu kutozingatiwa kwenye bajeti,” alisema.

Alisema pamoja na kuwepo kwa kanuni dhaifu, bado hata hizo zilizopo zimeshindwa kufuatwa kwa ukamilifu ambapo alitoa mfano wa kanuni ya 94  inayolitaka Bunge kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika Ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama Kamati ya Mipango katika kikao chake cha Februari ili kujadili na kuishauri serikali kuhusiana na Mpango wa Maendeleo utakaotekelezwa, hali inayolifanya bunge lifanye maamuzi ya kizembe.

Mnyika alisema kwamba udhaifu wa Bunge kwa mwaka huu umekuwa mkubwa zaidi katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/ 2013 sambamba na makadirio ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kupitishwa kwa siku moja, hali ambayo inachangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilifu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.

KUHUSU KATIBA


Akiongelea Katiba iliyopo, Mnyika, alisema imempa mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge na  kuwa inapotokea Bunge kuikataa bajeti ya serikali kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja Bunge, suala ambalo huwapa hofu wabunge wengi hususan wa chama kinachotawala na hivyo kuwafanya wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika kama ilivyotokea kwenye bajeti ya 2012/13.

Alisema udhaifu wa Bunge la sasa unachangiwa pia na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais ya kulivunja bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza mabadiliko katika bajeti na hivyo kuwafanya wasiwe na uwezo wa kubadilisha chochote.

Kwa mantiki hiyo, Mnyika, aliwashauri wananchi katika mchakato wa kutoa maoni ulioanza hivi karibuni kutoa maoni yatakayowezesha ukuu na uhuru wa Bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.

ATOA USHAURI KWA RAIS


Mnyika alimshauri Rais Jakaya Kikwete asome mwenyewe kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) za Juni 18 mpaka 22, mwaka huu na kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha Waziri wa Fedha  kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika bidhaa zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni ili kuondoa udhaifu uliopo.

KUTOLEWA BUNGENI

Mnyika alisema baada ya kutafakari kwa kina kisa cha kutolewa bungeni Juni 19 mwaka huu amefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati Bunge litakapoelekea kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013, ambapo pamoja na masuala mengine ataeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa kwa watanzania kutekelezwa na serikali.

Alisema aliamini na ataendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la rais kwa dhihaka na kwamba  kwa kuwa pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa chanzo cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika, Job Ndugai, bungeni wa kumhukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa, anakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment