


Baadhi ya Wakuu wa Wilaya wapya walioteuliwa na kuapishwa hivi karibuni wamekuwa wakifanya kazi katika ofisi za kata kutokana na kutokuwa na ofisi zao jambo ambalo limewafanya kufanya kazi katika mazingira magumu.
Wakizungumza na NIPASHE, mjini hapa kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wamesema hali hiyo imesababisha kufanya kazi katika majengo chakavu yasiyo na samani zinazolingana na hadhi yao.
“Mradi tumeshateuliwa, tunajua kuwa kazi ya uboreshaji wa maeneo ya kufanyia kazi itaendelea kufanyika taratibu, sasa ukianza kuulizia kuhusiana na ofisi nzuri ya kufanyia kazi hapa unajitakia matatizo bure,” alisema mmoja wa wakuu wa wilaya mpya.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kwa wakuu wa wilaya mpya ambao wilaya zao zipo karibu na wilaya za zamani wamekuwa wakiishi katika nyumba zilizopo katika wilaya hiyo na kwenda katika ofisi zao kila siku.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wakuu wa wilaya hizo kulazimika kusafiri umbali mrefu ukilinganisha na kama zingekuwepo nyumba katika wilaya hizo mpya.
Aidha, baadhi ya wakuu wa wilaya mpya wameonekana wakitumia magari binafsi kwa kile kilochodaiwa bado hawajapatiwa magari na wizara husika.
Juhuzi za kumpata msemaji wa wizara husika kuhusu suala hilo hazikuweza kufanikiwa baada ya kila alipotafutwa kuwa kwenye kikao.