


Adai siyo waliyokubaliana kwenye kikao, imechakachuliwa
Asema yuko tayari kufukuzwa uanachama kutetea wananchi
Siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, kuwasilisha bungeni bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013, mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Luhaga Mpina, ameibuka na kusema bajeti hiyo siyo ile waliyokubaliana katika kamati yao.
Aidha, Mpina ambaye ni Mbunge wa Kisesa (CCM), alisema yuko tayari kufukuzwa uanachama kwa kutetea maslahi ya wananchi waliomtuma kuwawakilisha bungeni.
Mpina aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana.
Bajeti iliyowasilishwa juzi na Dk. Mgimwa, ilionyesha kuwa matumizi ya kawaida katika bajeti hiyo ni asilimia 70 sawa trilioni 10.5 huku miradi ya maendeleo ikitengewa asilimia 30 ambayo ni sawa na sh trilioni 4.5.
Alisema fedha za ndani zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo katika bajeti hiyo ni trilioni 2.2 tu badala ya sh trilioni 2.7.
“Bajeti hii iliyowasilishwa inakiuka azimio la Bunge kwa kila mwaka wa fedha walau asilimia 35 itengwe kwa ajili ya maendeleo na kwamba kiasi kisichopungua sh trilioni 2.7 kutoka katika mapato ya ndani zielekezwe kutekeleza mpango. Hivyo bajeti ambayo imewasilishwa na Waziri wa Fedha si sahihi kwa mujibu wa mpango na maelekezo ya Bunge,”alisema.
Alisema kitendo cha serikali kutenga sh trilioni 2.2 badala ya sh trilioni 2.7 ambayo ni tofauti ya sh bilioni 500 kugharamia miradi iliyoainishwa katika mpango kumesababisha miradi mingi kutengewa fedha kidogo na mingine mingi kukosa fedha kabisa.
Alisema hii inaorodhorotesha utekelezaji na maana ya kuwa na mpango.
“Kibaya zaidi katika bajeti mapato ya ndani kwa sasa yameongezeka kwa sh trilioni 1.5 huku matumizi ya kawaida yakipanda kwa sh trilioni 1.9 wakati fedha za maendeleo zikipungua kwa sh bilioni 397.8 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2011/2012. “alisema na kuongeza:
“Hapa inajidhihirisha dhahiri kuwa serikali haina nia ya dhati ya kupunguza matumizi ya kawaida.” Alisema kwa kipindi kirefu serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kupunguza matumizi ya kawaida ili kuongeza kasi ya utoaji huduma na uwekezaji katika sekta zinazokuza uchumi na kupunguza umasikini lakini hivi sasa pato kubwa la taifa linatumika tu kuendesha serikali.
Alisema matumizi kama safari, posho, mafuta, ununuzi wa magari, samani, mawasiliano, sherehe, warsha, makongamano na mafunzo ya nchi yanayoweza kuepukika, kupunguzwa ama kuahirishwa.
Alisema wakati serikali ikiendeleza matumizi makubwa yasiyo ya tija Watanzania wanakufa kwa kukosa matibabu na ukosefu wa zahanati, dawa na waganga, maji safi na salama, elimu bora kutokana na upungufu mkubwa wa madarasa, umeme na reli, ukosefu wa viwanda vya kuongeza thamani kunakopelekea wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya kutupa.
“Mpango wa maendeleo ni mkataba kati ya wananchi na serikali lazima wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi tuulinde kwa nguvu zote na kwa gharama yoyote na kama mnavyoona katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango serikali inaanza kudharau mipango mizuri kama tulivyokubaliana,”alisema.
Alisema kuwa kwenye vikao vya kamati na wajumbe wenzangu waliniunga mkono na kwa pamoja waliitaka serikali ikafumue vitabu na kufanya marekebisho lakini serikali haikufanya hivyo bali waliendelea msimamo wao na kuja na visingizio vingi ambavyo havikubaliki kwamba eti kuna matumizi mengi yasiyo epukika.
Alisema watumishi watashindwa kutoa huduma, bajeti lazima isomwe sambamba na nchi za Afrika mashariki, maeneo ya utawala kuongezeka, hoja hizi hazina mantinki yoyote kwani ni kazi za kila siku za serikali na hata kipindi wanapitisha mpango wa maendeleo serikali ilikuwa inajua kuwa haya ni moja ya majukumu yake.
Alitoa mfano vitengo katika habari cha Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Fedha ambavyovimeongezewa fedha katika mafunzo nje ya nchi, mawasiliano na habari, safari za nje ya nchi, safari ndani ya nchi.
Alisema ongezeko hilo ni sh bilioni 4.7 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012, “je, hapa nia ya dhati ya kupunguza matumizi ya serikali iko wapi?
Alisema kunakosekana nia ya dhati kwasababu ukipitia mafungu yote ya fedha zaidi y ash bilioni 500 inapatikana bila shida.
Alisema kutokana na jambo hilo, aliomba mwongozo kwa Spika mara baada ya kusomwa kwa bajeti kwamba bajeti iliyowasilishwa siyo yenyewe na ombi lake lilikuwa ni kumtaka spika iridishwe serikalini ili ikaandaliwe upya kuliko kujadiliwa siku tano halafu ikataliwe.
Alisema spika alininyima muongozo huo kwa madai kuwa siku ya kuwasilishwa hakuna mwongozo na kwamba aliona ni uonevu kasababu katika kanuni zao Bunge toleo la 2007 hakuna kipengele kama hicho.
Hata hivyo, alisema kabla ya kuanza kujadiliwa kwa hotuba hiyo Jumatatu, ataanza kwa kuomba tena mwongozo wa Spika.
Alisema bajeti inayowasilishwa imekuwa ni hiyo hiyo ya kutenga asilimia 30 ya miradi ya maendeleo, haiwezi kulifikisha taifa linapotakiwa kwenda.
Mpina alisema hivi karibuni atawasilisha muswada wa sheria ambao utawezesha Bunge kuwa na kamati ya bajeti itakayoshughulikia uaandaaji, uidhinishaji na utekelezaji wa bajeti.
WABUNGE WA CCM WAJIPANGA
Wakati huo kikao cha Wabunge wa CCM kilichofanyika jana mjini hapa chini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, inaelezwa aliwasihi wabunge hao waipitishe bajeti hiyo.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoanza saa 5 asubuhi hadi saa 11.30 jioni , zilidai kuwa wabunge hao walilalamikia kodi zilizopandishwa katika bidhaa mbalimbali na kutaka zipunguzwe.
Chanzo chetu kimedai kuwa Kamati ya Hesabu, ilitarajiwa kuketi usiku jana kujadili vipengele mbalimbali vya kodi hizo ili ziweze kupunguzwa.
Aidha, wabunge hao wametaka kodi ya ushuru wa bidhaa za pamba zinazoingizwa viwandani zipunguzwe ili kuwezesha viwanda nchini kuzalisha malighafi hiyo badala ya kupeleka nje nchi.
Aidha, imedaiwa kuwa Mbunge wa Mbozi Kusini, Godfrey Zambi, alitishia kuwaadhibu mawaziri wanaochelewa kuingia kwenye vikao kama tishio walilolitoa kwa Waziri Mkuu katika kikao kilichopita cha kutokuwa na imani naye.
Kwenye kikao hicho, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba aliwataka wabunge waliosaini katika azimio la kumng’oa Pinda waadhibiwe.
Hata hivyo, hakuna aliyechangia hoja hiyo. Kangi Lugora(Mwibara) alipoomba nafasi ya kuelezea hakupewa ruhusa na Waziri Pinda.