



Juzi, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, akiwasilisha bungeni mjini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, aliliambia Bunge kuwa askari polisi 68 wamefukuzwa kazi kutokana na vitendo vya rushwa katika kipindi cha mwaka wa fedha uliomalizika Juni, mwaka huu.
Hali kadhalika, Waziri Dk. Nchimbi, alisema mbali ya askari hao 68 kutimuliwa kazi, lakini pia kulikuwa na kesi tisa za jinai ambazo zilikuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali hapa nchini zikiwakabili askari polisi huku askari wengine 15 uchunguzi wa malalamiko yao unaendelea.
Idadi ya askari hao 68 kufukuzwa kazi kwa kosa la rushwa kwa kipindi kimoja tu cha mwaka wa fedha, hakika imetushtua.
Aidha, Waziri Dk. Nchimbi, alisema katika mwaka wa 2011/12, jumla ya malalamiko 625 ya wananchi dhidi ya kero za rushwa yalishughulikiwa.
Ni ukweli usiopingika kuwa mara kwa mara baadhi ya askari wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi kuhusiana na vitendo vya rushwa.
Wanaongoza kwa kutuhumiwa kujihusisha na kudai na kupokea rushwa ni askari wa usalama barabarani ingawa pia hata askari wengine pia wamekuwa wakituhuhumiwa katika mazingira tofauti.
Kwa upande wa askari wa usalama barabarani, vilio vingi hutoka kwa madereva ambao hudai kuwa husumbuliwa mara kwa mara wawapo barabarani hata pale ambapo hawakustahili kufanyiwa hivyo.
Madereva hao hudai kuwa wanaposimamishwa na askari wa usalama barabarani, ni nadra mno kutopatikana na makosa hata kama gari halina matatizo na yeye mwenyewe ana kila kitu kinachohitajika.
Wanadai kwamba askari hao hulazimika kubuni kosa lolote lile kama njia ya kujenga mazingira ya wapewe rushwa ndipo waachiwe kuendelea na safari zao.
Kwa ujumla, yapo malalamiko lukuki ya madereva dhidi ya askari hao wa usalama barabarani.
Aidha, kwa askari wa kawaida, pia nao hulalamikiwa kwa mambo mbalimbali hususan wanapomkamata mtuhumiwa.
Inadaiwa kuwa baadhi ya askari wanapowakamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali, hutoa vitisho vyenye mwelekeo wa kutaka wapewe `kitu kidogo' na wanaotuhumiwa wakishindwa kutimiza hilo, basi hukimbizwa kituo cha polisi na hatima yake kufunguliwa mashitaka.
Pia baadhi ya askari hao wasio waaminifu wamekuwa wakidaiwa kuwabambikia kesi wananchi wasio na hatia.
Hali hii hutokana na wale wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza matakwa ya yule polisi aliyemkamata mtuhumiwa.
Tunafahamu kwa dhati kabisa kwamba si askari polisi wote wanaofanya vitendo hivyo, bali wapo wachache wasiowaaminifu ambao wanalipaka matope Jeshi la Polisi kwa ujumla.
Hakika wapo askari polisi ambao hufanya kazi zao vizuri tu kiasi cha kuwavuta hata wananchi wawakimbilie pale wanapopata matatizo.
Askari polisi wa namna hii, hawana budi kupongezwa na kuwasihi waendelee hivyo hivyo ili sifa nzuri ya Jeshi letu la Polisi, iendelee kudumishwa.
Pia utaratibu wa kuwazawadia askari wanaokataa kupokea rushwa katika utendaji wao wa kazi kama alivyosema Waziri Dk. Nchimbi, ni mzuri na unastahili
kudumishwa kwa lengo la kuwapa moyo askari waaminifu na waadilifu.
Lakini kwa wale wachache wenye tamaa wanapaswa kunyooshewa kidole ili warejee katika mstari sahihi ambao uongozi wa jeshi hilo pamoja na serikali, unasimamia.
Hata hivyo, kwa hatua hii aliyoitangaza Waziri Dk. Nchimbi ya kufukuzwa kwa askarri 68 kwa kosa la rushwa katika kipindi kimoja cha mwaka wa fedha, tunadhani kwamba inadhihirisha jinsi hatua mbalimbali zinavyochukuliwa na jeshi hilo katika kukabiliana na polisi wachache wenye nia mbaya ya kuchafua sifa nzuri za Jeshi la Polisi nchini.
Kwa hakika tunapongeza hatua hii na tungeshauri Jeshi la Polisi liendeleze vita hivyo dhidi ya wachache wanaotaka wananchi waamini msemo wa `samaki mmoja akioza, wote wameoza,' waondolewe kila wanapothibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa.