Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tuchunguze mahausigeli kabla ya kuwaajiri

1st July 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, leo tuzungumzie kuhusu wadada wa nyumbani yaani mahausigeli wetu, huku swali linalotuongoza likiwa ni “kwanini hausigeli aue mtoto wa mwajiri wake?” Hili ni tatizo kubwa na la kuogofya ndani ya familia na jamii yetu kwa ujumla.

Hebu sikia mfano huu kisha msomaji utoe maoni pamoja na ushauri wa nini kifanyike kuondokana na dhahama hii inayoathiri watoto wasio na hatia yoyote.

Wiki hii katika kipindi cha Wanawake Live kinachorushwa na kituo cha televisheni cha EATV, nilitizama kipindi hicho ambapo muandaaji wa kipindi, Bi. Kiria alikuwa akihojiana na wazazi wa mtoto anayedaiwa kuuawa na mfanyakazi wa nyumbani(hausigeli) katika mazingira ya kutatanisha. Habari ya kuuawa kwa mtoto huyo mdogo ilichapishwa katika gazeti la NIPASHE hivi karibuni.

Kilichonifurahisha katika kipindi hicho cha Tv ni jinsi Bi. Kiria na timu yake walivyoweza kufuatilia tukio hilo na hata kuandaa kipindi hicho ndani ya Wanawake Live. Baba na mama wa mtoto huyo(Mungu amweke roho yake peponi), walieleza kwa kina namna tukio hilo lilivyotokea na juhudi za kumsaka hatimaye kumkamata binti huyo.

Kingine kilichoonyesha umakini katika uandaaji wa kipindi hicho cha Tv ni jinsi walivyokwenda hadi kule alikokuwa akiishi kabla ya kuajiriwa na familia ile. Na huko wakagundua kuwa binti huyo pia aliwahi kufanya jaribio la kuchoma nyumba kwa mafuta ya taa ili kuwachomea ndani watoto wanne wa mama jirani yake.

Picha ikajionyesha dhahiri kuwa binti yule alikuwa ana vituko na inasemekana wakati anakwenda kukamatwa, alikuwa na hirizi jambo ambalo linaashiria kuhusisha nguvu za giza(ushirikina).

Mama mfiwa alionyesha huzuni nyingi kumkumbuka mwanae kifungua mimba ambaye alimwacha na hausigeli kwa kumuamini lakini akapoteza maisha kitatanishi. Kwa mujibu wa mama huyu, aliondoka kwenda kazini na kumuacha hausigeli na mtoto lakini huku nyuma hausigeli akaondoka na kumuacha mtoto pekee. Hausigeli huyu alikuwa amenunuliwa hata simu kwa ajili ya mawasiliano.

Akiwa kazini, mama akapigiwa simu kuwa nyumbani kuna tatizo arudi. Naye alipompigia hausigeni akamjibu ameondoka tangu asubuhi na kumuacha mtoto peke yake. Mama huyu kurudi nyumbani ndio akakutana na msiba wa mwanae.

Matukio ya aina hii ni mabaya sana. Lakini lipo jambo moja ningependa kutahadharisha kinamama na familia zetu kwa ujumla kuhusu mahausigeli. Wapo wale unaoletewa na wale ambao unakwenda kijijini kuwatafuta mwenyewe. Makundi haya mawili yana hatari zake. Nitazieleza zile nizijuazo na wewe msomaji utaongezea.

Tusichukue wafanyakazi hawa kwa kukurupuka tuwachunguze kabla ya kuwaajiri kwani wengine wamevaa ngozi ya kondoo kumbe mbwa mwitu.

Ni hivi, usikubali kuletewa msichana wa kazi ambaye hujui historia ya maisha yake. Kwa wale wanaopatikana mijini, wapo ambao kuwepo kwao ni baada ya kutoroka kijijini au eneo lingine nchini ambako alikuwa akifanya kazi ama akaiba au akafumaniwa na mume wa mama mwenye nyumba.

Mwingine pengine alishaua huko alikotoka au wala hajui shughuli za nyumbani, mwingine alikuwa akiuza baa kukamshinda na sasa anataka kuwa mfanyakazi wa nyumbani na kadhalika. Na hawa hutumia mbinu mbalimbali kuonyesha kuwa ni wa pole na watii ili wapate ajira.

Wengine wamekosana na waume zao kwa muda na kuja mijini kutembelea ndugu kisha kuamua kutafuta kazi za ndani kujikimu. Na baadhi huko wanakotoka huacha mtoto au watoto.

Kwa mfano yupo wifi wa rafiki yangu ambaye alipata msichana wa kazi ambaye alitokea Iringa. Huyu binti alikuwa ameolewa na kuzaa mtoto mmoja. Lakini wakatofautiana akaondoka kuja Dar kutafuta kazi. Akapata kazi kwa Afisa mmoja wa shirika la Kimataifa na mshahara mzuri.

Lakini kumbe bado alikuwa na mawasiliano na mumewe. Alipopata mishahara kwa miezi minne, hivi majuzi amemwomba mwajiri ruhusa akamuone ndugu yake mgonjwa hapo Chalinze. Kumbe alishamuaga mlinzi kuwa akipewa ruhusa hatarudi tena anamrejea mumewe.

Mpenzi msomaji, hawa mahausigeli ni watu wa kuangalia sana na hasa kujua historia zao. Kwa mfano msichana anayedaiwa kuua mtoto, baada ya kufuatilia ilibainika kuwa alishafanya jaribio la kuchoma nyumba kutaka kuua watoto wane. Na mashuhuda walitoa siri hiyo.

Kwa mantiki hiyo, wasichana wetu wa kazi tusikurupuke kuwaajiri, tuwachunguze kwanza, wengine ni mabedui, wasaliti hawana ubinadamu kwani ni wanafiki. Ndani ya roho zao ni ushetani mtupu.

Kwa upande mwingine, wapo wasichana wazuri na wenye moyo kweli wa kazi. Ila wanakumbana na viroja vya matajiri zao. Tukianzia kwa baba, wapo wenye tamaa za fisi wanawarudi kimapenzi. Wapo wanaoogopa na kutumbukia kwenye dhambi hiyo wengine yakiwashinda huamua kuondoka na pengine kwa kutoroka.

Kwa upande wa kinamama, hawa ndio wakati mwingine huwachochea ukatili. Hata kama binti alikuwa mpole hujifunza ujeuri kutokana na jinsi anavyonyanyaswa na mama mwenye nyumba. Wapo kinamama wenye hulka za matusi na wasiotaka majadiliano inapotokea kutofautiana na hausigeli wake.

Manyanyaso ya kila mara huweza kuwajengea chuki wasichana hawa na kuamua kutenda jambo baya kwa hasira. Kwa mfano msichana anadai mshahara wake wa miezi kadhaa bila mafanikio. Wengine uvumilivu huwashinda na kuamua kuondoka kwa mikwara kama vile kuiba vitu na wengine kujeruhi au kuua mtoto.

Matukio mabaya yanayofanywa na wasichana wa majumbani yanachangiwa na mambo mengi. Nimetaja hayo machache lakini msomaji mengine unayajua hivyo toa maoni tuelimishane, hatimaye tuweze kupata ufumbuzi. Wasichana hawa tunawahitaji lakini umakini katika kuwachagua yafaa uchukuliwe kwa kiwango cha juu kabisa, siyo kuajiri msichana ni msichana tu. Hapana.

Mpenzi msomaj, mchango wangu namalizia hapa ili nawe nikupe fursa ya kutoa maoni yako kuhusiana na mahausigeli tunaowaajiri majumbani mwetu.

Una uzoefu wowote juu ya jambo hili? Karibu changia maoni. Na ukiwa tayari, kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment