


.jpg)
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesisitiza kuwa serikali haitawachekea makandarasi wanaolipua kazi za ujenzi wanazopewa kwani watalazimika kuzirudia kwa gharama zao wenyewe.
Vile vile, ameahidi kuwa serikali italipa madeni yote ya wakandarasi kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha kwani imepata mkopo wa Sh. bilioni 300 kutoka serikali ya Uswis.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa mashauriano wa wakandarasi ulioratibiwa na Bodi ya Wakandarasi nchini (CRB) unaojadili namna ya kufuata sheria na taratibu za ujenzi.
“Wote mnajua kampuni ya Kajima siku chache zijazo inaanza ujenzi upya wa ile barabara ya Kilwa kwa gharama zake. Hivyo, inaeleweka wazi kwa sasa serikali haina mchezo na atakayebabaisha atajenga upya barabara,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Magufuli aliwasifu wakandarasi wazalendo na bodi ya CRB kwamba, wamekuwa wakijitahidi kufuata sheria na taratibu na kukamilisha miradi kwa wakati wanapopewa zabuni.