


Nimefuatilia kwa makini sana majadiliano ya waheshimiwa wabunge wakati wa mjadala wa kuijadili Bajeti ya serikali ya mwaka ujao wa fedha.
Tofauti na namna majadiliano hayo yalivyokuwa yakifanyika katika vikao vingine vya bajeti miaka ya nyuma, safari hii mfumo wa majadiliano umejidhihirisha muda mwingi kuongozwa na jazba za kisiasa, hasira, dharau, jeuri pamoja na kejeli badala ya kuijadili Bajeti hiyo na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa taifa.
Wakati wa Bunge la bajeti, wananchi wengi huelewa vizuri kuwa upo uwezekano wa ama kupata unafuu wa gharama za maisha au labda kuzidi kubanwa zaidi na ugumu wa maisha zaidi ya uliopo hivi sasa, yote yanategemea maamuzi ya busara yanayozingatia maslahi ya wananchi wote, ambayo waheshimiwa wabunge wanawajibika kuyatafakari kwa busara na hekima.
Kinyume cha hapo, athari za kubeza kwa makusudi mipango mizuri ya bajeti hii zitawaangukia wote, bila kujali tofauti zilizopo za vyama vya kisiasa. Hali halisi ndani ya majadiliano ya wabunge si ya kuridhisha sana kwani baadhi yao wameonyesha waziwazi kutokutoa ushirikiano wa namna ya kuweka mambo sawa.
Wananchi wanafuatilia kwa makini majadiliano yanayofanyika ndani ya jengo, na wanachoshuhudia hali ya hoja zitolewazo kama kweli zinazingatia uwakilishi wa hali za wananchi wengi walioko huko vijijini, wananchi wanaonekana kuingiwa na hofu ya wabunge wao kupoteza mwelekeo, baadhi ya wananchi wanaanza kudhani wabunge wao wapo kwa ajili ya kujipima uwezo wa kubishana bila hoja na kutafuta umaarufu wa kisiasa humo jengoni.
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) pia umetoa tamko ukieleza kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya wabunge kutumia Bunge kama sehemu ya malumbano ya kisiasa na kutambiana kwa elimu, vyeti na sifa binafsi badala ya kujadili miswada yenye manufaa kwa wananchi.
Mtandao huo pia umesikitishwa kwa baadhi ya wabunge wanaotumia lugha chafu ndani ya Bunge pamoja na vitendo kama vya kuchana nyaraka za mijadala Bungeni kwani tafsiri yake inaonyesha ni namna moja ya kuwatusi wananchi walala hoi ambao pia ni wapiga kura wao.
TGNP umewakumbusha waheshimiwa wabunge kuwa muda na nafasi wanayoipata katika kipindi hiki ni adimu waliyopewa kwa gharama kubwa za wananchi, haitaeleweka kama wabunge watatumia nafasi hiyo kwa kujadili maisha ya watu binafsi, kushambuliana vyama vya siasa, kufanya masihara na utani badala ya kujadili jinsi ya kusaidia na kuboresha maisha ya Watanzania walio wengi.
Wabunge wetu wanaelewa fika kuwa wajibu wao wakiwa ndani ya Bunge ni kufanya mijadala itakayoleta tija, mageuzi ya kiuchumi yatakayobadilisha hali duni na umaskini wa Watanzania walio wengi ambapo sasa hivi baadhi wanaishi kwa kupata mlo mmoja kwa siku na wengine wakibangaiza tu.
Wabunge bila kujali kama ni wa chama tawala au cha upinzani wanaelewa jukumu kubwa la kujikita katika kuchambua, kuijadili bajeti na hatimaye kuishauri serikali namna ya kuboresha na kuifanya itekelezeke kwa vipaumbele vilivyoko.
Isije ikawa kunajengeka kambi ya wabunge wanaong'ang'ania kuipitisha bajeti isiyotekelezeka ili kambi hiyo baadaye ipate jukwaa la kuishambulia serikali kwa kutofikia malengo, kama dhana hiyo ipo, basi inaweza kuzaa laana kutoka kwa wapiga kura wa kambi hiyo ambapo pia tafsiri yake itazaa migongano na mitafaruku isiyoisha.
Inaeleweka kuwa serikali ndiyo inayobeba wajibu wa kutekeleza kwa vitendo matumizi ya fedha zote zitakazoidhinishwa na Bunge, na itakapotokea serikali kuelemewa kwa ufanisi wa malengo ya miradi ya maendeleo kutokana na sababu zozote, wapo watakaotafsiri kuwa huo ni ushindi utakaowaongoza katika kujiimarisha zaidi.
Katika kufanikisha azma hiyo, kambi hiyo itakuwa imekwenda kinyume kabisa na matarajio ya wapiga kura wao, na kwa hakika athari zake kama zitakuwepo basi hazitachagua itikadi za vyama, badala yake zitatugusa wote.
Bunge letu lina wabunge wa kila taaluma, wapo wahandisi, maprofesa wa taaluma mbalimbali, madaktari, walimu, wanasiasa tu, makamanda wanajeshi, wafanyabiashara pamoja na wengine wa kada mbalimbali. Mjumuiko wa aina hiyo unatoa fursa ya kubadilishana mawazo kwa hoja tofauti na hatimaye wakafikia muafaka kwa niaba ya Watanzania wote.
Bunge lolote duniani lina jukumu la msingi la kutunga sheria, masuala ya bajeti pia ni ya kisheria. Katika kipindi hiki cha majadiliano ya bajeti ya serikali ni wajibu wa makundi ya wabunge wa taaluma zote kuona wanawajibika kuchangia maoni kwenye mijadala ya bajeti hii kwa maslahi ya maendeleo ya wananchi.
Baada ya wabunge kushambuliana wakati wa mijadala wiki hii, hatimaye juzi waliipitisha bajeti ya serikali kwa matumizi ya mwaka wa fedha utakaoanza Julai mosi mwaka huu.
Utaratibu wa kuipitisha bajeti ni kwa kura ambapo wabunge 225 waliikubali wakati wabunge 72 waliikataa ingawa wengine 52 hawakushiriki. Sehemu kubwa kama siyo wote walioikataa ni kutoka kambi ya upinzani isipokuwa tu Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo wa UDP aliyeikubali.
Miongoni mwa mapendekezo ambayo serikali ilikubaliana kufanya marekebisho katika bajeti hiyo ni Kodi ya Ongezeko la Thamani katika malighafi ya viwanda vya nguo, Tozo ya kuendeleza Stadi, kodi ya mapato kwa vijana wa 'bodaboda' na kulinda viwanda vya mafuta ya kula.
Maoni: 0715-047304 na 0762-233116