Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Sawia serikali kurejesha JKT lakini ijipange vema

17th July 2012
Print
Comments

Jana, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alitangaza bungeni mjini Dodoma azma ya serikali kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wanaohitimu elimu ya kidato cha sita hapa nchini.

Waziri Dk. Mwinyi, alifanya hivyo, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/13.

Katika hotuba yake hiyo, alisema serikali inakusudia kurejesha rasmi mafunzo ya JKT kwa vijana wanaohitimu elimu ya kidato cha sita kuanzia Machi, mwakani.

Dk. Mwinyi alisema makambi yaliyoandaliwa kwa sasa yana uwezo wa kuwachukua vijana 20,000 kwa mkupuo.

Hata hivyo, alisema kutokana na gharama za kuwatunza vijana hao na uendeshaji wake kwa ujumla, serikali itawachukua vijana 5,000 kwa majaribio kati ya wanafunzi 41,348 wanaotarajiwa kumaliza elimu ya kidato cha sita mwakani.

Waziri Mwinyi alifafanua kuwa vijana hao wataanza kuchukuliwa katika makambi ya JKT yaliyopangwa kuanzia Machi 7 hadi 16, mwakani na kuanza rasmi mafunzo Machi 17, mwakani ambapo watahitimu mafunzo hayo Agosti 16, mwaka 2013.

Hakika sisi tunasema hatua hii ya serikali ni nzuri na tunaiunga mkono kwa dhati kabisa.

Itakumbukwa kwamba Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa mwaka 1963 kwa lengo la kuwalea vijana kwa kuwafundisha umoja na uzalendo, kuwafundisha mbinu za uzalishaji mali na mafunzo ya ulinzi.

Aidha, mwaka 1972, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, lilipewa jukumu la kuiendeleza JKT na katika kipindi hiki, jeshi hilo lilikuwa likichukua vijana wa mujibu wa sheria kutoka mashuleni na kuwapatia mafunzo hayo.

Baada ya miaka mitatu Jeshi hilo lilianza kujishughulisha na shughuli za kilimo kama sehemu ya mafunzo hayo.

Hata hivyo, mafunzo hayo yalisitishwa baadaye mwaka 1994 kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa Mtanzania yeyote aliyebahatika kupitia mafunzo ya JKT, hapana shaka ataungana nasi kwamba yalikuwa yana umuhimu mkubwa mno kwa vijana wa Kitanzania.

Yalikuwa na umuhimu mkubwa kutokana na kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa jasiri, wakakamavu, wazalendo na wenye nidhamu ya hali ya juu.

Pia mafunzo ya JKT yalisaidia vijana wetu kuwa na umoja, kutobaguana kwa misingi ya ukabila au dini na vile vile yaliondoa tabaka la watoto wa matajiri na maskini.

Hali hiyo ilijidhihirisha dhahiri vijana hao waliomaliza mafunzo  na kuajiriwa kwenye mashirika ya umma (wakati huo), serikalini na hata katika makampuni binafsi.

Kwa ujumla, vijana waliopitia mafunzo ya JKT, walionekana tofauti kabisa na wale ambao hawakupitia mafunzo hayo kwa nidhamu, ukakamavu, uzalendo na hata moyo wa kujitolea.

Hii ndiyo maana sisi tunasema hatua hii ya serikali kurejesha tena mafunzo hayo ni mwafaka kwa mustakabali wa taifa letu.

Upo ushahidi kwamba baada ya mafunzo hayo kusitishwa mwaka 1994, mapungufu mengi kwa vijana yalianza kujitokeza hususan masuala ya nidhamu na hata ule moyo wa kujitolea kwa ajili ya ujenzi wa taifa lao.

Kurejeshwa kwa mafunzo hayo tutakuwa tumejiwekea akiba ya kutosha ya vijana watakaliosaidia taifa lao wakati wowote wa dharura.

Dharura hizi zinaweza kuwa ni majanga ikiwemo maafa ya mafuriko, ajali na matukio megine kama hayo.

Hata hivyo, tungependa kuishauri serikali kujipanga vema kuhakikisha inaboresha zaidi mazingira ya makambi ya mafunzo ya vijana hao tofauti na ilivyokuwa hapo awali ili vijana tunaowapeleka huko wasijione kama wamepewa adhabu na badala yake iwe ni kimbilio la wengi wanaomaliza shule.

Ni muhimu basi kwa serikali ikahakikisha kwamba inaboresha miundombinu katika makambi ya mafunzo kwa maana makazi yao na vitendea kazi ili vionekane ni vya kisasa zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kwa mfano, itapendeza zaidi vijana hao wakatumia matrekta na wanyama kazi kwa ajili ya kulimia badala jembe la mkono.

Ni kwa msingi huo basi, ndipo tunapoishauri serikali kujipanga vema kuhakikisha kwamba vijana hao watakapoanza mafunzo, wawe wamejengewa mazingira ya kuwa tayari kulitumikia taifa lao katika hali yoyote ile.

Lakini pia tungeishauri serikali kuhakikisha kwamba masomo la Ukimwi na maadili wanafundishwa makambini hasa kwa kuzingatia kuwa yatakuwa ni maeneo ya mkusanyiko mkubwa wa vijana wa aina mbalimbali na jinsia tofauti.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment