Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kamati ya Bunge yakataa bajeti ya Wizara ya Afya

11th June 2012
Print
Comments
Magreth Sitta

Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii imekataa kupitisha bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ikitaka irejeshwe na kuwepo mawasiliano upya kati ya wizara na serikali kwa ujumla kuangalia namna gani itatengewa fedha nyingi zitakazotosheleza upatikanaji wa dawa kwa wananchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Magreth Sitta, alisema bajeti hiyo imekiuka makubaliano ya azimio la Abuja, lililowakutanisha wakuu wa nchi za Afrika na kutaka asilimia 15 ya bajeti ya afya itumike katika huduma za jamii, lakini jambo la kushangaza kila mwaka bajeti ya wizara hiyo imekuwa ikishuka.

Alisema inashangaza bajeti hiyo haikugusia mgogoro wa madaktari na serikali ulioibuka hivi karibuni katika kuhakikisha kuwa kuna kipengele kilichotengwa kutatua baadhi ya matatizo ya madaktari.

Sitta aliyasema hayo baada ya kutembelea Kituo cha Afya cha Mlandizi, mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya kuiwezesha kamati hiyo katika ufuatiliaji na utekelezaji wa shughuli katika wizara hiyo.

Pia kuona jinsi gani huduma kwa wagonjwa zinaboreshwa kupitia mpango wa malipo ya motisha kwa watumishi wa sekta ya afya.

Vile vile, kamati hiyo imekataa Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuitaka iboreshe kitengo cha Ukaguzi shuleni kwa kuwa fedha zilizotengwa ni chache ikilinganishwa na tatizo lililopo.

Aidha Kamati hiyo iliukumbuka mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba  Muhimbili eneo la Mloganzira ambao tayari wafadhili wametoa Dola milioni 76, lakini umekwama kutokana na kusubiri mchango wa serikali.

Mwisho



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment