Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yanga yapigania Na.2 kwa APR leo

20th July 2012
Print
Comments

Kipigo cha 5-0 walichopata Wau Salaam kutoka kwa Atletico ya Burundi jana kilimaanisha kwamba Yanga imefuzu kucheza hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na washindi wa jana na APR ya Rwanda huku timu hiyo ya Sudan Kusini ikiaga mashindano ikiwa imefungwa jumla ya mabao 19-1 katika mechi tatu za Kundi C.

Timu moja tu kutoka kila kundi ndiyo inayoaga mashindano. Timu tatu-tatu kutoka katika makundi A na C yenye timu nne-nne zitaungana na timu mbili kutoka Kundi B, lenye timu tatu, kucheza robo fainali zitakazoanza Jumatatu.

Nafasi ya pili katika Kundi C ndiyo ya juu zaidi ambayo Yanga wanaweza kumaliza baada ya Atletico kufikisha pointi 7 kwa ushindi wa jana uliofutia vipigo vya Wau Salaam vya 7-0 na 7-1 kutoka kwa APR na Yanga.

Hata hivyo, ili kumaliza katika nafasi ya pili, Yanga yenye pointi 3, ni lazima iifunge APR iliyo na pointi 4 katika mechi yao ya kufungia makundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam saa 10:00 leo.

Baada ya kuanza na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Atletico, Yanga walifufuka katika mechi yao ya pili dhidi ya Wau Salaam kwa ushindi wa 7-1 Jumanne na wanahitaji kuthibitisha leo kuwa hawakubahatisha kuifunga timu hiyo changa ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza kutokea katika nchi ya Sudan iliyotawaliwa na vita kwa miaka mingi kabla ya kujitenga.

Mshambuliaji wa Yanga, Mganda Hamisi Kiiza ambaye aliibuka mchezaji wa kwanza kufunga 'hat-trick' katika mashindano hayo mwaka huu wakati walipochakaza Wau Salaam, amesema amedhamiria kuifungia timu yake mabao mengi ili itetee vyema ubingwa.

Kiiza aliiambia NIPASHE kuwa amefurahi kufunga mabao matatu katika mechi moja na kwamba jambo hilo limemuongezea kujiamini mbele ya lango.

"Nina furaha na ninataka kuiongezea Yanga furaha katika mechi inayokuja, nawajua APR, ni mechi ya ushindani lakini nimejipanga kuwakabili," alisema mshambuliaji huyo.

Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kwamba mechi hiyo ya leo itakuwa ni ya ushindani kwa sababu timu zote mbili zina wachezaji wenye uwezo na wanaotaka kushinda.

"Timu nzuri zinapokutana mechi huwa nzuri zaidi, tumejipanga na tunajua kwamba kila upande unahitaji kushinda," alisema beki huyo ambaye pia huichezea Zanzibar kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji.

Mapema wiki hii kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alisema kwamba licha ya kuhitaji matokeo mazuri leo, atapendelea kumaliza akiwa nafasi ya pili kwenye kundi hilo ili kumkwepa mtani wake, Simba kwenye hatua ya robo fainali.

Naye kocha wa APR, Ernie Brandts alisema amewaandaa vizuri wachezaji wake kwa ajili ya mechi hiyo ya kesho ambayo ni wazi itakuwa na ushindani lakini akaongeza kwamba haihofii Yanga licha ya kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Katika mechi ya utangulizi leo saa 8:00, Ports ya Djibout itacheza dhidi ya URA yenye pointi sita ambayo ndio kinara wa kundi A na tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali.

Mafunzo ya Zanzibar ilikaa kileleni mwa Kundi B kutokana na kufikisha pointi mbili baada ya sare yao ya pili dhidi ya Tusker ya Kenya wakati zilipotoka 0-0 jana.

Ilitoka pia sare ya 1-1 dhidi ya Azam. Timu itakayoaga kutoka kundi hilo itajulikana Jumamosi wakati Azam itakapocheza dhidi ya Tusker zote zikiwa na pointi moja-moja.



 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment