Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Fainali ya Simba, Azam kupigwa Dar kesho

11th July 2012
Print
Comments
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba na mshindi wa pili wa ligi hiyo, Azam zitakutana katika mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la Urafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kesho.

Jumamosi mashabiki na wadau wa soka wa Zanzibar walionekana kulalamikia maamuzi ambayo yalikuwa bado hayajatangazwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ya kuhamishia fainali hiyo jijini Dar es Salaam na walidai kwamba endapo jambo hilo likifanyika 'watasusa' kuingia viwanjani katika mechi za ligi na nyingine zitakazofanyika visiwani.

Michuano ya Kombe la Urafiki ilikuwa ikifanyika visiwani Zanzibar na maamuzi ya kuhamisha fainali hizo yalitangazwa jana baada ya timu zilizofika hatua hiyo zote kuwa zimetokea Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Haji Ameir, alithibitisha kuwapo kwa mabadiliko ya mchezo huo na kusema kwamba wameona itakuwa vyema kuwapa nafasi mashabiki wa timu hizo walioko Dar es Salaam kuziona kabla ya kuanza kwa mashindano ya Kombe la Kagame.

Katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Simba na Azam zilitoka sare lakini timu zote mbili hazikutumia wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali za makocha wao.

Wachezaji wa Azam wanaoichezea timu ya taifa (Taifa Stars) wakiwemo Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Aggrey Morris na Salum Abubakar walibaki jijini Dar es Salaam kwenye programu maalumu ya kocha Stewart Hall wakati kocha wa Simba, Milovan Cirkovic aliamua kuwapa nafasi chipukizi wengi kuonyesha vipaji vyao.

Yanga ilienguliwa katika mashindano hayo na ZFA kutokana na kupeleka timu ya vijana badala ya wakubwa ambayo ilibaki Dar es Salaam kujiandaa kutetea ubingwa wake wa Kombe la Kagame.

Yosso wa Yanga walicheza mechi moja dhidi ya Jamhuri kutoka Pemba na walilala magoli 3-2.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment