Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Baraza la Mitihani hawako makini katika utendaji

10th June 2012
Print
Comments

Maofisa na wasaidizi wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), inavyoonekana hawako makini katika utendaji wao wa kazi.

Hali hiyo sasa inatia shaka kwani inaondoa uaminifu. Kwamba, ikiwa watu hawa hawako makini, wanawezaje kuaminika katika usahihishaji wa mitihani wakati wanafanya makosa ya kimsingi sana.

Mfano hai wa kosa la wazi la maofisa na wasaidizi hao wa NECTA lisilomkinika nililolishuhudia ni hili.

Wiki iliyopita, niliona barua iliyomhusu mtu wangu wa karibu aliyehitimu kidato cha sita katika shule moja ya sekondari nchini mwaka huu.

Barua hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kwenye bahasha ya rangi ya kaki, ilikuwa inatokea NECTA.

Nyuma ya bahasha hiyo kuna alama ya muhuri uliogongwa kwenye bahasha hiyo. Muhuri huo una maneno yanayosomeka kwa lugha ya Kiingereza yanayotambulisha barua hiyo kuwa inatoka NECTA.

Maneno hayo yanasomeka hivi: ‘National Examination Council’. Yakimaanisha: ‘Baraza la Mitihani la Taifa’.

Ukiangalia kwa makini maneno hayo ya Kiingereza yaliyomo kwenye huo muhuri, kwa wanaojua vyema lugha ya Kiingereza, wanaweza kugundua kuwa yana kosa la wazi iwapo walioyaandika walikusudia yatafsirike kwa lugha ya Kiswahili: ‘Baraza la Mitihani la Taifa’.

Kosa hilo linatokana na kukosekana herufi ‘s’ mwisho wa neno ‘Examination’.

Kukosekana kwa herufi hiyo, kunaondoa herufi ‘i’ inayopaswa kuwapo kati ya herufi ‘M’ na ‘t’ kwenye neno ‘Mitihani’.

Herufi ‘i’ ikiondoka kati ya herufi hizo, inaleta tafsiri ya ‘Mtihani’ na hivyo kusomeka kwa lugha ya Kiswahili: ‘Baraza la Mtihani la Taifa’, badala ya ‘Baraza la Mitihani la Taifa’.

Kama nilivyotangulia kueleza hapo juu kwamba, kosa kama hilo haliyumkiniki kutendwa na watu makini wanaotarajiwa kuwapo NECTA.

Kwa sababu watu hao hawawezi kufikia kukosea kwa kiwango hicho kwenye kitu kidogo tu kama muhuri.

Ikiwa ni hivyo, swali la kujiuliza ni hili. Hivi hawa maofisa wa NECTA na wasaidizi wao, hawajaona kosa hilo kwenye maandishi ya muhuri huo? Au wameona lakini wameamua tu kuacha kwa makusudi?

Kama jibu ni ndiyo, hoja inarudi palepale. Kwamba NECTA hawako makini katika utendaji wa shughuli zao.

Kama wameona kosa hilo wakaamua kuacha tu au wakadharau, inadhihirisha wazi pia kuwa hawako makini. Na kwa hiyo, kamwe hawawezi kuaminika.

Tukiachana na kosa hilo la kwenye muhuri, kosa lingine la wazi na la msingi limeonekana pia katika maelezo ya moja ya barua za NECTA niliyoiona.

Barua hiyo ilisainiwa Mei 5, mwaka huu na mmoja wa maofisa waandamizi wa NECTA kwa niaba ya katibu mtendaji wa baraza hilo.

Barua hiyo inakiri kuwa yalifanyika makosa katika usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita ya mwaka huu. Sasa NECTA inarekebisha na kuwasiliana na mamia ya wanafunzi kuwajulisha makosa hayo.

Katika barua hiyo, wanafunzi hao wameombwa kurejesha vyeti vyao vya matokeo ya awali ili wapewe vyeti vingine vipya vyenye marekebisho.

Kutokana na makosa hayo, mmoja wa wanafunzi ambaye barua yake nimeiona, alipewa daraja la tatu kwa makosa, lakini baada ya marekebisho, alipanda hadi daraja la pili!

Ikiwa hali ndiyo hiyo, hali ikoje kwenye mambo, ambayo yanahitaji umakini zaidi? Mfano, uwekaji wa herufi za alama na madaraja mbalimbali.

Je, maofisa hawa wa NECTA na wasaidizi wao, hawafanyi makosa kama hayo? Mfano, mtu kaandika ‘D’ badala ya ‘C’ au ‘D’ badala ya ‘B’?

Jibu sahihi na la haraka haraka la swali hilo, ni kwamba maofisa na wasaidizi hao wa NECTA hawako makini. Na inawezekana katika kuweka alama hizo huwa wanasomeana.

Kwa hali hiyo, yafaa NECTA wakazingatia yafuatayo. Mosi, wanapaswa kujua kwamba, suala la usimamiaji mitihani ni nyeti. Hivyo, wanapaswa kuajiri watu waliofaulu vizuri katika fani ya takwimu.

Pili, yafaa wakafanya usimamizi wa karibu kwenye mchakato wote wa usahihishaji wa matokeo na upangaji.

Tatu, yafaa wakafanya uhakiki kwa umakini zaidi. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, hivi sasa wanafanya hivyo, lakini si kwa umakini.

Ndio maana nasema Baraza la Mitihani la Taifa hawako makini katika utendaji wa shughuli zao.

Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656.

Baruapepe: muhibu72@yahoo.co.uk

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment