



Inampasa mtu mwendawazimu kushangilia, kukejeli, kuipa nafsi furaha ya moyoni pale binadamu mwingine anapotendewa ilivyo kinyume cha haki za binadamu.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, amekutwa na dhoruba, nchi imezizima, hofu imetanda, unyama umefanyika!
Vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, vimetangaza, vimechapisha picha na habari zinazoashiria nuru ya thamani ya amani inatoweka!
Nguli wa nyimbo za uhamasishaji katika kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT) cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Komba, aliwahi kuimba akayataja maneno hayo.
Akaendelea kusema “amani Afrika imetoweka leo, amani duniani imetoweka leo kumbe Tanzania, imejichimbia.’
Kwamba nuru ya thamani ya amani iliyopotea kwenye mataifa mengi duniani, hapa nchini ilikuwa imejichimbia.
Sina hakika leo hii, Komba ambaye ni Mbunge wa Mbinga Magharibi, akipewa nafasi ya kutumbuiza, anaweza kuuchagua wimbo wenye kibwagizo hicho, kisha akauimba kwa majigambo. Sidhani!
Kutekwa, kupigwa, kujeruhiwa, kisha kutupwa kwenye pori la Mabwepande, alivyofanyiwa Dk Ulimboka, kunaongeza viasharia vya kupotea kwa nuru ya thamani ya amani.
Zipo hoja nyingi zinazotolewa kuhusu tukio hilo, zipo hisia tofauti zinazoelezwa na ipo miunganiko ya matukio inayofanywa kwa lengo la kutaka kuhalalisha utambuzi wa wahusika wa kadhia hiyo.
Lakini msingi hapa ni tukio zima, kwamba lilimpata kiongozi wa madaktari waliokuwa wanashiriki mgomo, wakisimamia madai mbalimbali.
Kwa hali hiyo, umoja wa madaktari na hatua ya kusimamia kile wanachokiamini, ulikuwa msingi wa nguvu na ujasiri wa viongozi wao, akiwemo ‘kijana wetu’ Dk Ulimboka.
Si kwamba Dk Ulimboka ana nguvu nyingi, ana misuli na umbile la kutisha ama vinginevyo, la hasha.
Nguvu za Dk Ulimboka ni matokeo ya umoja, mshikamano na msimamo wa madaktari. Kwa wanaoamini kwamba ‘kumshughulikia’ Dk Ulimboka ni kuwashughulikia madaktari, anapotoka.
Kuamini hivyo, ni sawa na anayetaka kujiaminisha kuwa kwa kumuua aliyekuwa kiongozi wa kundi la Al Queda, Osama Bin Laden, kungekuwa suluhu ya kuushinda ugaidi duniani.
Sitaki niwianishe tukio la Dk Ulimboka na lile la Osama aliyeuawa na majeshi ya Marekani Mei mwaka jana. Lakini ki-mantiki yanaweza kufanana hasa suala la ‘kumshughulikia’ mtu ili kupata suluhu ya tatizo la kijamii linapohusika.
Hivi sasa Dk Ulimboka amelala kitandani, anauguza maumivu makali aliyoyapata baada ya kipigo, kinachohusishwa na harakati za kudai maslahi ya madaktari na mazingira bora ya huduma za afya kwa Watanzania.
Kama Dk Ulimboka angepigwa baada ya kufumaniwa mahali popote chini ya jua, asingegusa hisia za watu kiasi cha ilivyo sasa. Kama Dk Ulimboka angepigwa baada ya kushikwa akikwapua simu ya mtu anayetembea barabarani, tukio hilo lisingekuwa na mguso sana zaidi ya kudhalilika.
Kama Dk Ulimboka angekuwa amehusika kumlaghai binti aliye mwanafunzi ili wakafanye mapenzi, kisha akakutwa na ‘vijana wa mtaani’ na kumshushia kipigo, asingeipendeza jamii. Angesononesha.
Dk Ulimboka amekutwa na kadhia hiyo katikati ya harakati alizoziongoza kudai haki za madaktari na mazingira bora ya huduma za afya.
Kwamba katika orodha ya madai hayo, yalikuwepo masuala ya upatikanaji dawa na vifaa vya tiba. Dai hilo linaigusa jamii pana ya Watanzania.
Iwe iwavyo, kuwepo orodha ya madai yakiwemo ambayo hayajafanyiwa kazi, ndiko kumeibua mgomo wa madaktari unaohusishwa kwa karibu na tatizo lililomkuta Dk Ulimboka.
Bila shaka, pasipo kuathiri maslahi binafsi ya madaktari, umma umechangia kwa yaliyomkuta Dk Ulimboka, ikiwa kusudio ni kumnyamazisha dhidi ya kuendeleza harakati za madai hayo.
Kwa maana kama isingekuwa haki za madaktari kwa ujumla wao, kama isingekuwa mazingira bora ya huduma za afya, Dk Ulimboka asingefungua kinywa chake, angekosa mamlaka ya kufanya hivyo, yasingemfika yaliyomfika.
Damu ya Dk Ulimboka imeshamwagika, anaweza kuongezewa nyingine lakini ile ya asili imeshazama ardhini. Ikamuacha akiendelea kuuguza maumivu makali. Pole sana Dk Ulimboka.
Wakati nikizitafakari hekaya zinazoendelea kutolewa kuhusu tukio hilo, huku upepo ukivuma zaidi upande wa mgomo wa madaktari, nikayakumbuka maandiko matakatifu.
Ilipoandikwa, “ni heri mtu mmoja afe kuliko kuungamiza ulimwengu wote.” Dk Ulimboka hajafa, amejeruhiwa vibaya ili jamii ya Watanzania ipate mazingira bora ya huduma za afya, moja ya hitaji la msingi katika haki za binadamu.
Inawezekana kupitia kipigo na maumivu ya Dk Ulimboka, serikali ikaielekea sekta ya afya na kuamua kuboresha upungufu uliopigiwa kelele na madaktari katika sekta ya afya. Atakuwa mfano wa mkombozi.
Dk Ulimboka anapaswa kuyavumilia mateso ambayo hakuyategemea. Kuna wakati atalia ama kuliliwa na ndugu, jamaa na marafiki wanapomuona akiuguza maumivu. Asisoneke.
Kwa vile amekutwa na hayo akiwa kwenye harakati za kudai haki zenye maslahi kwa umma, asihuzunike. Ni bora zaidi kwa binadamu kama Dk Ulimboka, kupoteza viungo vya mwili, kuliko angeshiriki hujuma zenye kuiangamiza ‘dunia ya Watanzania.’
Mwisho wa siku, huduma za afya zitaboreshwa, hatua itakayochochewa na damu ya Dk Ulimboka iliyomwagika. Inaweza isiwe mwaka huu, lakini kwa namna yoyote, itakuwa vigumu kuzungumzia uwepo wa huduma bora za afya pasipo kulitaja tukio la kutekwa na kuteswa kwake.
Hapo ndipo kila mgonjwa atakaporidhika na mazingira bora ya huduma bora za afya kwenye hospitali za umma, atapata faraja, atapona kwa maana kupitia damu ya Dk Ulimboka, yote yatawezekana.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com.