Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wachezaji Simba wawekwa kitimoto

20th July 2012
Print
Comments
Kikosi cha Simba

Licha ya kupata ushindi wa magoli 3-0 juzi dhidi ya 'wachovu' Ports ya Djibout, wachezaji wa Simba, waliwekwa kitimoto juzi na benchi lao la ufundi linaloongozwa na Mserbia Milovan Cirkovic ikiwa ni mara tu baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.

Wachezaji wa imu hiyo walichukua zaidi ya saa moja kumsikiliza kocha Cirkovic na wasaidizi wake ambao walikuwa wakielezea makosa mbalimbali yaliyofanyika katika mechi hiyo ambayo wengi walitarajia kuona wawakilishi hao wa Tanzania Bara wakipata ushindi mnono dhidi ya wapinzani ambao walipokea kipigo cha mabao 7-0 katika mechi yao ya utangulizi dhidi ya S Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa kawaida, kila baada ya kumalizika kwa mechi, makocha huzungumza kwa muda mfupi na wachezaji wao. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti juzi kwani Simba walichukua muda mrefu kuzungumza, huku Cirkovic akidaiwa kuchukizwa na kiwango cha chini kilichoonyeshwa na wachezaji wake.

"Mwalimu alikuwa anaeleza mapungufu ambayo hakuyatarajia na pia baadaye wachezaji tulikuwa tukijaribu kueleza kilichofanya mchezo uwe mgumu tofauti na ilivyotarajiwa," alisema mmoja wa wachezaji wa Simba.

Mchezaji huyo alisema vilevile kuwa wachezaji wengi walishindwa kucheza kwenye kiwango chao kutokana na wapinzani hao kuwakaba zaidi ya wawili kwa wakati mmoja.

Cirkovic aliliambia gazeti hili kwamba ameshukuru timu yake imeshinda, lakini hajaridhishwa na kiwango cha wachezaji wake katika mechi mbili za awali za michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Alisema kwamba wachezaji wake wanatakiwa kubadilika zaidi na kuweka umakini kwenye mechi zote bila kudharau wapinzani.

"Hawakunifurahisha jinsi walivyocheza, nahitaji kufanya kazi zaidi ili timu iwe ya ushindani, sijui kwa nini wako hivi, tunaelekea kwenye ushindani zaidi huko mbele," aliongeza kocha huyo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment