Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Niyonzima: Naja kesho na kasi mpya

25th June 2012
Print
Comments
Kiungo wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa mashindano ya Kombe la Kagame timu ya Yanga, Haruna Niyonzima.

Kiungo wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa mashindano ya Kombe la Kagame timu ya Yanga, Haruna Niyonzima, kutoka Rwanda anatarajiwa kurejea nchini kesho Jumanne ili kujiunga na wachezaji wenzake ambao tayari wameshaanza kujifua kwa ajili ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo.

Niyonzima aliondoka nchini mara baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kumalizika Mei 6 mwaka huu na kurejea kwao Rwanda kujiunga na timu yake ya taifa maarufu Amavubi.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Kigali, Niyonzima alisema kuwa anatarajia kurejea nchini akiwa na nguvu mpya ili kuisaidia Yanga iweze kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame na akiwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa (Amavubi) amefanya mazoezi kwa muda mrefu.

Niyonzima alisema kwamba licha ya Amavubi kutopata matokeo mazuri katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza fainali za Dunia na kutolewa kwenye safari ya kuelekea Afrika Kusini mwakani katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika lakini wachezaji wote wako kwenye viwango vya juu.

"Niko fiti, narejea Dar nikiwa tayari kuja kufanya kazi, naamini msimu ujao utakuwa na mafanikio kwetu (Yanga)," alisema kwa kifupi kiungo huyo ambaye kwenye tuzo za TASWA alibwagwa na Emmanuel Okwi wa Simba.

Alisema kuwa mashindano ya Kombe la Kagame mwaka huu yatakuwa magumu zaidi kwa sababu klabu nyingi zitakuwa na wachezaji walioiva kutoka kwenye timu za taifa.

Mashindano ya Kagame yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yataanza kufanyika Julai 14 hadi 29 na yatashirikisha timu 12 za ukanda huu ikiwemo Sudan Kusini ambayo ni mwanachama mpya.

Pia kutakuwa na timu mbili zilizoalikwa kutoka nje ya CECAFA lakini kutokana na kukosekana wadhamini, klabu zote zimetakiwa kujigharamia usafiri.

Wakati huo huo, ujio wa mshambuliaji, Meddie Kagere, wa Polisi Rwanda bado ni kitendawili kutokana na mchezaji huyo kuwa na mkataba na timu yake hiyo unaotarajiwa kumalizika Julai 4 mwaka huu.

Pia Kagere ambaye ni raia wa Uganda pia anatakiwa na St. George ya Ethiopia huku akiweka wazi kwamba ndoto yake ni kuchezea klabu kubwa barani Afrika na baadaye Ulaya akipata nafasi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment