Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

EU yaimwagia Tanzania Sh. bilioni 99

22nd July 2012
Print
Comments
  Ni kwa ajili ya maji safi na kuimarisha miundombinu ya maji taka

Umoja wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania zaidi ya Yuro milioni 51(Sh.bil.99), zitakazowezesha kuwapatia maji safi pamoja na kuimarisha miundombinu ya majitaka kwa wakazi zaidi ya 500,000 wa miji ya Kigoma, Lindi na Sumbawanga.

Kwa ujumla Umoja wa Ulaya umetoa Yuro milioni 126 (sawa na Sh bilioni 245) kusaidia ujenzi wa barabara vijijini, miradi ya maji, kuimarisha asasi za kiraia (Azaki) Zanzibar na kuijengea uwezo wa kiutendaji ofisi za EU nchini kwenye, mijadala, usimamizi wa rasilimali na mafunzo ya watumishi.

Makubaliano hayo ya kuisadia Tanzania yamesainiwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Maendeleo wa EU Andris Piebalgs na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, mbele ya Rais wa Kamisheni ya EU Jose’ Manuel Barroso na Rais Jakaya Kikwete.

Ni mara ya kwanza kwa Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Barroso na Piebalgs, kuzuru Tanzania ambapo pia Rais huyo alitoa salamu za pole kwa taifa kufuatia ajali ya meli ya Zanzibar.

Katika taarifa ya pamoja ya Marais hao, walisema Yuro milioni 51.51 sawa Sh bilioni 99 zitatumika kwenye maji katika mikoa hiyo mitatu, ambapo ujenzi wa mtandao wa bararaba kuu umetengewa Yuro milioni 45 sawa Sh. bilioni 88 na ule wa barabara za vijijini umepatiwa Yuro milioni 22 sawa na Sh bilioni 43.

Viongozi hao walibainisha kuwa Yuro milioni tatu sawa na Sh bilioni sita zimetolewa kuimarisha shughuli za Azaki za Zanzibar wakati Yuro milioni 5 sawa na Sh bilioni 10 zimeelekezwa kwenye miradi ya kujenga uwezo wa wataalamu wa kusimamia miradi na kazi za EU nchini kila eneo likitengewa Sh. bilioni 4.9.

Akizungumzia miradi ya maji, Rais Kikwete alisema fedha hizo zitawezesha kuwapatia wakazi wa miji ya Kigoma, Lindi na Sumbawanga maji safi na salama na kuondoa tatizo sugu la maji katika maeneo hayo.

Pia alisema mji wa Mbeya nao umo kwenye programu ya kuupatia maji safi na kwamba uzinduzi wa mradi huo unanza leo.

Kwa upande wa barabara fedha hizo zitawezesha kukarabati zaidi ya kilometa 200 za barabara na kuwezesha zipitike muda wote.

Kikwete aliongeza kuwa Tanzania ilijiunga na EU mwaka 1975 na kuanzia hapo imenufaika na misaada ya umoja huo kupitia mikataba ya Lome na Cotonou inayoziunganisha nchi za Afrika, Caribbean, Pacific na EU.

“Tanzania imeanza kunufaika na misaada ya EU tangu mwaka 1975 na imeweza kupata misaada ya zaidi ya Yuro bilioni 1.8 sawa na Sh trilioni 3.8, ” alisema.

Barosso kwa upande wake alisema EU ina nia ya kuisaidia Tanzania kuwekeza kwenye kilimo kupitia mradi wa Ushirikiano wa Kuzalisha Chakula baina ya EU na mataifa tajiri dunia ya G8 maarufu kama G8 Food Alliance.

Alisema watashirikiana na serikali kwenye miradi ya kilimo kwenye ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Aliongeza kuwa umoja huo utashirikiana na Tanzania kwenye maeneo ya kupambana na ugaidi, uharamiaji wa baharini, kuzalisha nishati na kupunguza umaskini kwenye maeneo kadhaa pamoja na kilimo.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment