Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Padri Mapunda: CCM imeshindwa kutatua matatizo

25th June 2012
Print
Comments

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetakiwa kijiandae kutoka madarakani  kwa kuwa wameshindwa kusimamia haki za wananchi na kuwafanya kuendelea kuishi katika maisha magumu pamoja na kushindwa kudhibiti  mfumuko wa bei.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na  Padre Baptiste Mapunda wa Kanisa Katoliki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Farijika Afrika Mashariki, wakati alipokuwa akiendesha ibada katika Kanisa la Mtakatifu Karoli  Lwanga la Yombo Dovyo, Dar es Salaam.

Alisema kuwa serikali ndiyo chanzo cha matatiz,o hali ambayo imepelekea taifa kuwa katika hali mbaya huku wananchi wakiendelea kuishi katika maisha magumu.

“Nchi inakoelekea ni kubaya, Watanzania wanakaa bila kujitafakari, hii hali itaendelea hivi mpaka lini?” alihoji na kuendelea:  “Ni lazima tutafute viongozi ambao watakuwa na uchungu na maisha ya wananchi na sio wanaojali mali zao.”

Alisema ameshangazwa kuona watu wakichoma makanisa huku serikali ikisema kuna amani wakati sio kweli na kuwa hakuna hatua zilizochukuliwa.

Alisema CCM imekuwa ikijitapa kuwa haitaondoka madarakani, lakini kutokana na kutokuwajibika lazima itaondoka kwa kuwa haiwezekani taifa liendelee kuwa katika hali mbaya kutokana na serikali iliyoko madarakani.

“Chama ambacho hakitaweza kuondoka madarakani ni cha Yesu peke yake ila CCM ijiandae kuondoka kije chama kingine ambacho kitatuongoza kwa umakini na taifa kuwa katika hali nzuri, matatizo yote unayoyaona yameifikisha taifa katika hali mbaya yamesababishwa na serikali iliyoko madarakani,” alisema.

Aidha, alisema yaliyojitokeza katika bunge la wiki iliyopita ilikuwa ni aibu kubwa kwani wabunge walikuwa wakitukanana hali ambayo ilionyesha picha mbaya kwa wananchi.

Alisema viongozi kama hao ambao wanaonyesha ubabe pamoja na matusi katika Bunge hawana haja ya kuchaguliwa katika kipindi kijacho.

Akizungumzia bajeti, alisema ameshangazwa kuona wabunge wa CCM wakiunga mkono huku wakijua kabisa kuwa bajeti hiyo haiwalengi wananchi wa kawaida.

Alisema bajeti iliyopitishwa ni mbaya na imelengwa kwa ajili ya maslahi ya watu matajiri ma kwamba maskini haiwasaidii, jambo ambalo alisema litasababisha kuongezeka kwa hali ngumu ya maisha.

“Sukari ipo bei ya juu kwa kilo ni Shilingi 2,000 wakati inatengenezwa hapa hapa, wameshindwa kudhibiti tatizo la mfumuko wa bei halafu wanatengeneza bajeti ya kuwangonga wananchi,” alisema Padre Mapunda.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment