


.jpg)
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika tamasha la utoaji tuzo za wanamichezo bora nchini litakalofanyika leo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo la kila mwaka linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), limedhaminiwa na kampuni ya bia ya Serengeti Breweries (SBL).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema mshindi wa jumla katika tamasha hilo ataibuka na zawadi ya Dola za Marekani 8,000 (ambazo ni sawa na Sh. milioni 12), cheti pamoja na kikombe.
"Washindi wa tuzo nyingine watapata kikombe na Sh. milioni 1 kwa kila mmoja," alisema Pinto.
Aliongeza kuwa kila kitu kuhusu maandalizi kimeshakamilika na kwamba kwa upande wa burudani bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo itatumbuiza.
Pinto alisema wanamichezo watakaopewa tuzo leo ni wa riadha, wavu, netiboli, kuogelea, tenisi, judo, kikapu, soka, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu (ridhaa), gofu (wa kulipwa), baiskeli na kriketi.