


Kitendo kinachotokea mara moja baada ya miaka kumi ni tukio linalohitaji maandalizi makini, inawezekana wanaoratibu kufanikisha hilo wanahitaji mtandao mkubwa wa wadau mbalimbali katika kutoa hamasa na elimu ya namna ya kufanikisha.
Sensa ya Watu na Makazi hapa nchini itafanyika tarehe 26 Agosti, 2012, zimebakia siku 47 tu kuanzia leo kabla ya siku hiyo muhimu kitaifa. Jukumu letu kwa pamoja ni kushiriki kikamilifu siku hiyo na kutoa ushirikiano kwa wataohusika na utekelezaji wake.
Katika makala kama hii ya wiki iliyopita, niligusia maeneo muhimu ya jitihada zilizofanywa na ambazo bado zinaendelea kufanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuwahamasisha wananchi kujitokeza mwezi ujao kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi, pia nilitoa historia fupi ya umuhimu wake kitaifa wa Sensa ijayo.
Leo nitatoa kwa ufupi maana ya maswali yatakayoulizwa siku ya Sensa na namna wananchi tunavyotakiwa kutoa ushirikiano katika kuyajibu maswali kutoka kwa wasimamizi wa Sensa.
Maswali yatakayoulizwa yamezingatia pia kuwatoa hofu na wasiwasi unaoweza kuwa umejengeka kwa baadhi ya wananchi ambao kutokana na mila, desturi au sababu nyingine wanaiangalia Sensa ya Watu na Makazi katika mtazamo tofauti na ule wa Kitaifa ambao ni kukusanya takwimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Yapo madodoso yaliyotayarishwa na yenye maswali kulingana na aina ya taarifa au takwimu zinazotakiwa kukusanywa.
Kuna Dodoso la Jamii ambalo litakusanya taarifa za huduma za Jamii kama vile shule, hospitali, vituo vya afya, masoko, huduma za fedha, majosho, vyanzo vya maji, mazingira, matukio ambayo yaliwahi kutokea katika Jamii hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambayo yanaonekana kuwa kero kwa Jamii pamoja na masuala ya maafa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Lipo Dodoso lingine ambalo nalo litakuwa na maswali yatakayoulizwa juu ya jina la Mkuu wa Kaya, majina ya watu wote waliolala katika kaya hiyo katika usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti, 2012 pamoja na kujua uhusiano wa watu hao na mkuu wa kaya.
Maswali mengine yatakayoulizwa yatahusu jinsi, umri, hali ya ulemavu, hali ya ndoa, uraia na mahali anapoishi, anaposhinda mwanakaya na kama anacho cheti cha kuzaliwa nk.
Yapo maswali mengi ya kawaida ambayo mwananchi haitampa shida kuyajibu endapo tu atatoa ushirikiano kwa watakaohusika na Sensa hiyo, na maswali yote yatakuwa na lengo la kukidhi mahitaji mbalimbali ambayo Taifa linahitaji hivi sasa na baadaye kwa ajili ya upangaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Kila mwananchi anawajibika kuyajibu kwa usahihi na ufasaha ili Sensa ya mwaka huu itoe Takwimu zitakazoisaidia serikali kufanya mipango thabiti ya maendeleo ya wananchi wake.
Pamoja na mchakato unaoendelea wa kuwaelimisha wananchi kuhusu Sensa ya mwaka huu, wapo baadhi ya wananchi ambao tayari wameanza kuchanganya kati ya Sensa ya Watu na Makazi na Vitambulisho vya Taifa.
Baadhi yao wanaanza kushangaa wanaposikia Sensa itakayofanyika tarehe 26 Agosti mwaka huu, kwa yale maeneo ambayo tayari makarani wanaowaandikisha wananchi kwa ajili ya vitambulisho wameshapita, baadhi yao wanadai kuwa hilo ndilo zoezi la Sensa inayozungumzwa na kwamba tayari wameshahesabiwa.
Dhana hiyo pia inahitajika ifafanuliwe kwa baadhi ya wananchi ambao hata faida za kufanyiwa Sensa bado hawajazifahamu vyema. Ni wajibu wa serikali za mitaa za huko wanakopita makarani wa vitambulisho vya Taifa kuwatahadharisha wananchi kuwa hiyo siyo Sensa yenyewe.
Ukiangalia namna maswali yatakayoulizwa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi yalivyopangwa, utakuta yanaelekeza kujua mwananchi anavyoishi, idadi ya watu wasio na ndoa kwa ajili ya kuwapangia mahitaji yao maalum, kufanya mchanganuo wa uraia uliopo nchini, kutambua ukuaji wa miji, idadi ya wananchi walio na vyeti vya kuzaliwa.
Pia maswali hayo yanalenga kujua idadi ya watoto yatima ili Taifa liweze kupanga mipango sera ya watoto yatima, idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika pamoja na viwango vya elimu, ukosefu wa ajira, nguvu kazi ya Taifa na maeneo yanayotoa ajira, kiwango cha uzazi nchini, wastani wa umri wa kuishi, kiwango cha umaskini katika kaya, uboreshaji wa sera za kilimo na ufugaji ana masuala mengine mengi. Ni katika mpango huu wa Sensa ya Watu na Makazi ambapo serikali inaweza kujipangia mikakati mbalimbali ya kuwakwamua wananchi wake baada ya kujua hali halisi ya umaskini wa wananchi wake.
Ufafanuzi wa maswali hayo utasaidia pia kwa Serikali kufuatilia na kutathmini MKUKUTA na MKUZA, ambazo ni Dira za Taifa za Maendeleo kwa mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na mwaka 2020 kwa Tanzania Zanzibar, pia ufafanuzi huo utasaidia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Malengo ya Milenia ya mwaka 2015.
Tunao muda wa zaidi ya mwezi mmoja na nusu wa kujipanga vizuri kabla ya siku ya Sensa yenyewe, nafasi hii ni muhimu kwa viongozi wa serikali za mitaa kuendelea kuwahamasisha wananchi kuwepo katika makazi yao ili kazi hii iwe rahisi na yenye ufanisi wa kutosha.
Ni wajibu wetu sote kushirikiana katika azma hii ya Taifa ambayo si kwa ajili ya kujua idadi tu ya Watanzania, bali pia iweze kutoa dira ya mipango ya maendeleo ya Taifa kwa miaka mingi ijayo.
Maoni tuwasiliane: 0715-047304 na 0762-233116