Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Shiboli atua Polisi Moro

30th June 2012
Print
Comments
Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Coastal Union, Ally Ahmed Shiboli

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Coastal Union, Ally Ahmed Shiboli, ametua katika timu iliyorejea ligi kuu ya Bara, Polisi Morogoro, huku akisisitiza kuwa wale wanaodhani ameisha wamsubiri kumuona msimu mpya ukianza Septemba mwaka huu.

Shiboli, aliyetemwa na Coastal sambamba na wachezaji wengine nane, alisema amefikia makubaliano na Polisi Moro iliyopanda daraja na timu nyingine mbili za Mgambo Shooting na Prisons-Mbeya.

Mfungaji huyo bora wa ligi kuu ya Zanzibar misimu ya 2008-2009 na 2009-2010, alisema anaamini bado ana kiwango kikubwa cha soka ndio maana hata Polisi wameamua kumsajili ili aitumikie.

Alisema hata hivyo kuthibitisha hilo mashabiki wanapaswa kusubiri kuona ligi ikianza na kuonyesha makali yake ya kutupia mipira nyavuni, sifa iliyomfanya Simba impapatikie na kumnyakua misimu miwili iliyopita baada ya kung'ara na timu ya taifa ya Zanzibar.

"Sitaki kusema lolote kwa sasa, ila mashabiki wasubiri kuniona ligi ikianza nikiwa na Polisi Moro," alisema.

"Naamini uwezo wangu bado upo juu ila sijapata mahali pa kutumiwa vema kama ilivyokuwa Duma ama Coastal niliyoichezea nusu msimu na kuifungia mabao."

Shiboli alisema kwa kutambua changamoto kubwa aliyonayo, amekuwa akitumia muda huu wa mapumziko kujifua mwenyewe ili kujiweka fiti zaidi kabla ya msimu haujaanza baadae.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment