Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Serikali ijifunze kuwa sikivu

19th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Kuanzia jana hadi keshokutwa wabunge wataijadili kwa kina bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2012/13 kisha kuipitisha ili ianze kutumika ifikapo mwaka mpya wa fedha Julai Mosi.

Serikali imetangaza kuwa inakusudia kutumia kiasi cha Sh. trilioni 15 mwaka kwa mwaka huo, kati yake Sh. trilioni 10.5 ni matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 4.5 kwa ajili ya maendeleo.

Tangu kuwasilishwa Alhamisi wiki iliyopita kumekuwa na maoni mbalimbali juu ya bajeti hii, kikubwa ni serikali kukiuka azimio la Bunge kuhusu visheni ya maendeleo ya Tanzania 2025 ambayo ilipitishwa na Bunge la sasa kwamba ni lazima fungu la maendeleo la bajeti ya serikali liwe ni walau asilimia 35 ya fedha zote. Katika bajeti hii serikali imetenga asilimia 30 tu.

Bajeti ya mwaka unaokuja ni kubwa zaidi kuliko inayomalizika ambayo serikali ilipanga kutumia Sh. trilioni 13.5, kwa maana hiyo ongezeko la Sh. trilioni 1.5 lilitarajiwa lijionyeshe likielekezwa kwenye sekta ya maendeleo kwa kuwa kufanya hivyo ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na umasikini.

Kwa muda mrefu sasa kila bajeti ya serikali inapowasilishwa bungeni kumekuwa na mvutano unaojiainisha katika mgongano wa kimikakati, wakati baadhi ya wabunge wakiiona serikali imezidisha matumizi ya kawaida na hivyo kuibatiza bajeti hiyo kuwa ni ya kula, serikali kwa upande wake imekuwa ikijitetea kuwa hakuna njia nyingine ya kujinasua katika hali hiyo.

Katika mwelekeo wa namna hii, serikali imekuwa inalaumiwa kuwa inajiruhusu kubebeshwa lawama kwa kuwa haionyeshi kwa dhati kutambua changamoto za kweli kitaifa ndiyo maana imekuwa inakuja na bajeti ya kula mwaka baada ya mwaka.

Kwa mfano, wapinzani wa bajeti ya sasa wanasema kuwa, wakati mwaka huu unaomalizika serikali ilitenga Sh. trilioni 8 kwa ajili ya matumizi ya kawaida kati ya Sh. trilioni 13.5 zilizokuwa zimetengwa kwa bajeti nzima, kwa maneno mengine mwaka huu wa fedha unaomalizika, serikali imetenga fedha za maendeleo Sh. trilioni 4.5, inakuwa je ikarejea kiasi hicho hicho mwaka unaokuja?

Serikali ilisemwa sana mwaka jana, na kilele cha kusema ni kukataliwa kwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo ilionekana wazi kuwa serikali haikuwa na mpango wa kweli na unaotekelezeka wa kuondoa taifa katika tatizo sugu la mgawo wa umeme; serikali iliondoa makadirio ya wizara hiyo na kwenda kujipanga upya; hata hivyo mipango hiyo bado inalegalega hadi sasa.

Serikali imekiri mara kadhaa kwamba inatumia fedha nyingi katika matumizi ya kawaida bila sababu za msingi kabisa; miongoni mwa maeneo ambayo yanakula sana fedha ni posho, semina, safari, manunuzi ya samani za bei mbaya, magari na matumizi mengine mengi ambayo kwa hakika hayajawahi kuwa na tija katika kukabiliana umasikini wa watu wa nchi hii.

Ni kwa maana hii tunapotafakari mjadala unaoendelea bungeni Dodoma, tunashindwa kujua kama kweli serikali ni sikivu na inajali matatizo ya wananchi kwa jinsi inavyogawanya rasilimali za taifa hili.

Ukweli huu unapata uzito zaidi kwa sababu wakati mwaka wa fedha unaomalizika matumizi ya kawaida yalikuwa ni Sh. trilioni 8, mwaka unaokuja zimepanda kwa wastani wa Sh. trilioni 2, wakati fedha za fungu la maendeleo limebakia pale pale.

Balaa inayonyemelea taifa ni kwamba wakati mwaka wa fedha unaokuja serikali imeendelea kutenga fedha zile zile za mwaka unaomalizika, ni wazi kuwa hakutakuwa na miradi mipya ya maendeleo itakayoanzishwa kwani hata ile iliyoanza mwaka huu unaokwisha na ile ya zamani zaidi, fedha zake hazikutoka.

Hii ni sawa na kusema kuwa katika mwaka ujao wa fedha hakuna matumaini ya kuondoa taifa katika kero za kimsingi za barabara, reli, maji  na viwanja vya ndege.

Tunasema wabunge ni wawakilishi wa wananchi, wanachozungumza bungeni mara nyingi kinakuwa na mashiko kwa maana ya kukabiliana na shida za wananchi kwa maana hasa ya shida za wananchi, ni katika hali kama hii tunaishauri serikali safari hii iote masikio, isikilize na kufanya mabadiliko chanya katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13 ili kuharakisha maendeleo ya taifa hili na watu wake.
 

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment