Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Simba kutaja kikosi leo

16th June 2012
Print
Comments
Geofrey Nyange 'Kaburu'

Wakati Simba ikitarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi kujiandaa na Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, uongozi wa klabu hiyo leo unatarajiwa kutangaza majina ya wachezaji waliowasajili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema watawatangaza leo wachezaji wapya waliowasajili kwa ajili ya kuichezea timu hiyo msimu ujao.

"Tunajiandaa kuingia kambini hivi karibuni, lakini kesho (leo) tutangaza majina ya wachezaji wetu wapya pamoja na wale wa zamani ambao wataitumikia timu yetu msimu ujao pamoja na mashindano mengine ya kimataifa," alisema Kaburu.

Alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukifanya mambo yake kwa utulivu bila papara na umekamilisha kazi hiyo hivyo leo wanachama wa Simba watawajua wachezaji wao.

Aidha, alisema utata wa mchezaji Kelvin Yondan aliyemwaga wino Yanga pia wauacha kwa shirikisho la soka (TFF) ambalo ndiyo litatoa uamuzi, lakini akasisitiza kuwa mchezaji huyo ni mali ya Simba.

Katika hatua nyingine, Kaburu amewapongeza wachezaji wawili wa klabu hiyo waliopata tuzo za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) na kudai walistahili kutokana na uwezo wao.

"Sisi kama viongozi tunawapongeza wachezaji Shomari Kapombe na Emmanuel Okwi kwa kutwaa tuzo na hii imetokana na juhudi zao," alisema Kaburu.

Wachezaji hao waliibuka na na tuzo hizo ambapo Okwi alipewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kimataifa anayecheza nchini wakati Kapombe aliibuka na tuzo mbili za Mchezaji Bora Chipukizi na Mwanamichezo Bora wa Mwaka.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment