Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tanzania yapata vifaa vya majanga baharini

16th June 2012
Print
Comments
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Ahmad Kilima

Tanzania imepokea vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 192 vilivyotolewa na wadau mbalimbali wa masuala ya mafuta wakiwemo Kampuni ya Mafuta ya Total (T) ili kuchukua hadhari ya kulinda mazingira ya baharini na pwani.

Matukio ya meli kumwaga mafuta baharini yanasababishwa na meli za mizigo kama za mafuta na za abiria ambako kumeelezwa kuhatarisha mazingira ya baharini kwa kuua viumbe hai wake.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kwenye hafla ya kupokea vifaa maalumu vya kukabilina na uharibifu huo wa mazingira unaosababishwa na kumwagika kwa mafuta baharini, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Mngodo, alisema vifaa hivyo ni faraja kwa Tanzania.

Alisema vifaa hivyo vitasaidia katika kutekeleza mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imetia saini kama ile ya kuzuiya uharibifu wa mazingira baharini.

Kwa mujibu wa Mngodo, vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuyakabili majanga ya aina hiyo yanapoikabili nchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Ahmad Kilima, alisema wanakusudia kuwa na vifaa vya aina hiyo katika bandari za Mtwara, Tanga na Zanzibar.

Alisema vifaa hivyo vina thamani ya sh. milioni 192 (paundi 77,999) ambavyo vimetolewa na wadau mbalimbali wa masuala ya mafuta wakiwemo Kampuni ya Mafuta ya Total (T).

Kilima alisema Tanzania iko katika hatari kubwa ya kupata majanga ya kumwagika kwa mafuta kutokana na kuwepo kwa meli nyingi za abiria na mizigo zinazotumia bahari ya Hindi lakini pia huagiza mafuta kutoka nchi za nje.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Ukanda wa Bahari ya Hindi (IOC), Raj Prayag alisema vifaa hivyo vimegawanyika katika makundi tofauti.

Baadhi ya vifaa hivyo alivitaja kuwa ni mota na vifaa vya kunyonya mafuta yaliyomwagika na matoroli matatu ya kubeba vifaa hivyo. Imeelezwa kuwa Tanzania ilikuwa na vifaa vya kukabiliana na matukio hayo, lakini si vya kisasa ikilinganishwa na vilivyotolewa jana.

Hafla hiyo iliwashirikisha viongozi mbalimbali wanaohusika na masuala ya mafuta, majeshi ya majini na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari na wafanyakazi wa Bandari na wale wa Sumatra.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment