


Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliahidi kukuletea mada kuhusu jinsi watu wanavyotafuta wachumba na changamoto wanazokumbana nazo nikitolea mfano mazungumzo niliyonasa toka kwa familia mbili wakielezea mchakato waliopitia hadi sasa wakajikuta wanaitwa ni baba na mama watoto.
Katika mada ile nilijadili wale wachumba wanaojikuta wako mbali kwa muda na mambo yanayojitokeza hata wakati mwingine uchumba ukavunjika kabla ya kuhitimisha mkataba wa ndoa.
Nilitoa mfano wa kijana aliyekuwa akilalamika kuwa mchumba wake alipata kazi mikoani na tokea wakati huo akiwasiliana naye hapokei tena simu. Wapo wasomaji waliompa ushauri na kabla sijahitimisha makala haya nitaweka ushauri wako.
Naam. Hivi majuzi nilikuwa sehemu na marafiki zangu nyakati za jioni tukipata vinywaji. Ilikuwa ni mtu na mkewe na baba mwingine alikuwa akimsibiri mkewe ambaye alikuwa njiani akitokea kazini.
Katika mazungumzo, likajitokeza suala la namna kinababa hawa walivyowapata wake zao. Familia hizi marafiki zikawa na maelezo tofauti kuhusu namna walivyokutana hadi kufikia kufunga ndoa.
Baba katika familia moja akaanza kwa kusema; Kama lipo jambo ambalo sitalisahau ni jinsi nilivyompenda mama watoto tokea tukio chuoni Mzumbe. Wakati nikimchumbia, alianza kuolewa mdogo wake.
Nikaalikwa kwenye sherehe. Wakati wa mahari wazazi upende wa binti wakadai mahari ya vitu mbalimbali. Jambo hili sikulifurahia kwani naamini ukimtolea mwanamke mahari unakuwa umemnunua na mimi katu sikutaka kumununua mke wangu.
Jambo hili nililipinga nikamwambia mchumba wangu kwamba katu mimi sitatoa chochote. Na kweli nilikomaa sikutoa chochote baada ya kuwaelimisha wazazi wa mchumba wangu. Hatimaye nilimuoa kwa sherehe kubwa inayokumbukwa hadi leo. Na ndoa yangu imedumu kwa rehemu za Mungu wetu haina ufa wa aina yoyote.
“Hivi ndoa za kutoa mahari, nyingi zimepata misukosuko kutokana na mke kuuzwa kwa mahari kama nyama dukani. Siyo utaratibu mzuri”, anamaliza kusema baba huyu.
Kidogo akadakiza mama wa familia ya pili akasema, “Mimi nilipata shida sana. Nilikuwa nafanya kazi benki ambako watu walinisumbua sana wakinitaka uchumba…walikuwemo mameneja na wafanyakazi wenzangu lakini wote niliwakataa.
Kama kuna kitu sitasahau ni jinsi nilivyosumbuliwa wakinitaka uchumba nikatamani kuacha kazi. Hata hivyo Mungu alivyo mkubwa nikaja kukutana na mume wangu huyu baada ya maombi sana na tumeishi vizuri bila mkwaruzano wowote”.
Mpenzi msomaji, kwa mifano hii miwili, unaweza kuona jinsi watu wanavyotoka mbali katika kujenga mahusiano hadi wanajikuta katika nyumba moja kama mke na mume na watoto wao. Ama kwa hakika, mke mwema au mume mwema hutoka kwa Mungu.
Wako watu wengi wenye historia nzuri nyingine zikisikitisha kuhusu jinsi walivyojikuta wanaoana. Unakuta wamepitia misukosuko mbalimbali lakini hatimaye wakawa washindi. Wengine wanaishi hadi sasa ni wazee, wengine maisha ya ndoa yaliishia njiani ama kwa kukatishwa na kifo au ndoa kuvunjika kutokana na ugomvi usioisha, ufukara wa baba mama akamkimbia, fumanizi zinazoishia ndoa kuvunjika na kadhalika.
Mpenzi msomaji, hata hivyo vipo vigezo mbalimbali ambavyo vinahitaji kuzingatiwa ikiwa mtu anataka kuoa au kuolewa na hivyo kuimarisha au kudumisha ndoa na mahusiano kwa jumla.
Kwa mfano, wanawake wazuri kwa sura na umbo ambao tabia na mienendo yao hairidhishi huwa katika nafasi kubwa ya kuishi bila kuolewa, na kwa bahati mbaya zaidi wanawake wengi wanaohesabika kuwa ni wazuri, tabia na mienendo yao ni ya kutilia mashaka.
Wanaume wengi huvutiwa na wanawake hao kujenga uhusiano nao hasa wa kimwili tu na si vinginevyo, na ndio maana wanawake wazuri kwa sura na umbo wanalo soko kubwa sana kwa wanaume, lakini huishia kuchezewa zaidi kuliko kuolewa.
Wanaume nao kwa upande wao wamejenga dhana kwamba wanawake wazuri sana sio wa kuoa na hivyo kuwaogopa. Wanaamini kwamba wanawake wazuri sana ni wasumbufu, kitu ambacho kina ukweli kwa kiasi fulani.
Baadhi ya wanaume huwa na hisia kuwa wanawake wazuri sana kwa sura na umbo huwasababishia waume zao maradhi ya moyo, shinikizo la damu na wakati mwingine hata kuwafanya kupata matatizo fulani ya kiakili. Hiyo inatokana na waume hao kuwatilia shaka wake zao kuchukuliwa na wanaume wengine wakati wowote kutokana na uzuri wao.
Hata hivyo, wanawake wazuri nao huwapeleka puta waume zao kwa kujijua ni wazuri na soko lao liko juu hali inayofanya waume zao kuwanyenyekea wakihofia kuachwa.
Ndio maana haishangazi kuona kuwa wale wanawake ambao watu wamekuwa wakiamini kuwa ndio wabaya kwa sura au umbo lakini tabia na mienendo yao ni mizuri, ndio wanaoolewa na hata ndoa zao zinadumu, tofauti na wale wanaoonekana kuwa ni wazuri kwa sura na umbo huku tabia na mienendo yao si mizuri, ndoa zao hazina umri mrefu.
Je, msomaji wangu, je wazijua tafrani za kusaka wachumba? Kama unacho cha kusimulia kuhusu maisha yako ya ndoa au ya ndugu yako, rafiki yako, kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.
Wasalaam.