Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tukatae uhalifu sekta ya dawa

20th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Miongoni mwa hujuma ambazo zinafanyiwa watu wa nchi hii na kuonekana kama ni kawaida tu ni kulishwa ama dawa bandia, zilizokwisha muda wake au ambazo hazikidhi viwango.

Vitendo hivi ingawa vinapewa majina lainilaini, kimsingi ni mauaji. Uuzaji wa dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu iwe zimekwisha muda wake wa kutumiwa au chini ya viwango, ni sawa kabisa na kulisha watu sumu. Ni kitendo cha kutekeleza uhalifu wa mauaji ama wa mara moja au polepole.

Dawa iliyokwisha muda wake ni rahisi sana kugeuka kuwa sumu mbaya ambayo ina uwezo wa kuua mara moja, lakini dawa feki ambayo haijafikia kiwango humfanya mgonjwa asipone maradhi yanayoumsumbua hivyo kuvifanya vijidudu kuwa sugu na hivyo kumsababishia mateso makubwa mgonjwa na mwisho wake kifo kinaweza kumpata.

Matukio ya kuzagaa kwa ama dawa bandia nchini au ambazo zimemaliza muda wake wa matumizi yamekuwa ni ya kawaida, wiki iliyopita Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilikamata shehena ya dawa bandia ambazo zilikuwa zimeingizwa sokoni katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Katika msako huo, watu 13 walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na utengenezaji, uagizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa hizo bandia katika mikoa ya Kanda hiyo, sehena iliyohusu dawa za aina mbalimbali.

Hiyo siyo operesheni ya kwanza kufanywa nchini ambayo hufanywa na TDFA kwa kukusanya taarifa za kiitelijensia wakishirikiana na Jeshi la Polisi, hivyo kupata taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa kinyume cha Sheria ya Chakula, Dawa na vipodozi ya mwaka 2003.

Kuthibitisha uhalifu ulivyoingilia sekta ya dawa na ufamasia kwa ujumla, pia zilikamatwa dawa za serikali za kutibu kifua kikuu na ukoma ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka binafsi, pamoja na dawa moto ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka ya dawa baridi.

Taarifa ambazo ziliripotiwa katika vyombo vya habari jana, gazeti hili likiwamo, miongoni mwa dawa bandia zilizokamatwa ipo yenye majina mawili tofauti kwenye lebo moja ambayo ni “Praziquantel 600mg na Amodiaquine Hydrochloride 200mg, ikiwa kwenye makopo 117 yenye ujazo wa vidonge 100 kila moja na imeghushiwa kuwa imetengenezwa na kampuni ya Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) Limited ya jijini Arusha.

Dawa nyingine iliyokamatwa ni yenye jina la kibiashara la “Sulxine & Primine na jina halisi Sulphadoxine & Pyrimethamine (SP) ikiwa kwenye makopo yenye ujazo wa vidonge 1,000 na imeghushiwa kuwa imetengenezwa na kampuni ya Micro Labs Limited ya nchini India; kadhalika TFDA ilifanikiwa kukamata lebo kadhaa za dawa bandia aina ya Ephedrim, Dioerythro na Erythromycin ambazo baadhi yake ziliwahi kukamatwa na mamlaka hiyo siku za nyuma yakiwamo makopo matupu 62 yasiyokuwa na lebo yoyote, makopo 54 yenye lebo za dawa tofauti, mifuko ya kufungia dawa katika makopo, chupa yenye kemikali ya kufutia maandishi na nyaraka mbalimbali pia zimekamatwa kwenye nyumba ya kulala wageni iliyopo Igoma jijini Mwanza.

Ingawa wito ulitolewa kwa wenye maduka, zahanati na vituo vya afya waliouziwa dawa hizo wazisalimishe mara moja katika ofisi za TFDA na waache kununua zinazotembezwa mikononi, ukweli unabakia kwamba biashara ya dawa za bindamu, mifugo na hata kilimo imeingiliwa na matapeli waliokubuhu.

Vyombo vya dola mkoani Mwanza vimedai kuwa biashara haramu ya dawa za binadamu inaendeshwa na kundi la wafanyabiashara laghai wageni ambao wamejipenyeza nchini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao wanashirikiana na raia wa Tanzania kufanya uhalifu huu unaochukua maisha ya raia wenzao kwa tamaa ya fedha chafu.

Tulipata kusema huko nyuma kwamba adhabu zinazotolewa dhidi ya wahalifu wauzaji dawa bandia na zilizokwisha muda wake ni nyepesi mno na hazifanani hata kidogo na kosa linalotendeka. Uuzaji wa dawa wa aina hii ni mauaji na adhabu ya kosa la mauaji  inajulikana.

Tunafikiri kama taifa tufikie mahali na tuseme basi dhidi ya uhalifu na kila aina ya ushenzi unaofanywa kuangamiza maisha ya watu wetu na kikundi kidogo cha watu wenye tamaa ya kujipatia utajiri katika njia chafu kama uuzaji wa dawa bandia na zilizokwisha muda wake.

Tukatae sasa na tutengeneze sheria kali kwa makosa haya sawa na mauaji au kukutwa na dawa za kulevya ili kuwatia adabu wote wanaohusika.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment