


Michuano ya kila mwaka ya kuvumbua vipaji kwa vijana jijini Dar es Salaam ya 'Street Cup' yanaanza leo yakishirikisha timu 12.
Mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo utakuwa kati ya timu ya Sunburst dhidi Tabata Junior kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Tabata.
Mratibu wa michuano hiyo Rogers Peter alisema lengo la michuano hiyo ya kila mwaka ni kuvumbua vipaji vya vijana ambavyo baadaye huwapa ajira kwa kusajiliwa na timu mbalimbali.
Peter ambaye pia ni Mwenyekiti wa timu ya Moro United iliyoshuka kutoka ligi kuu ya Bara msimu huu alisema kuwa mafanikio ya michuano hiyo huko nyuma ni kupata vijana ambao waliipandisha Moro United kucheza ligi kuu.
"Mbali na timu zitakazofungua dimba leo, timu nyingine zinazoshiriki michuano hii ni Pentax, Ubaya Ubaya, Matumbi, Mtambani, Azimio, Remnant, Umoja Road, Liwiti, Mbuyuni na Polisi Kota," alisema Peter.
Aidha, alizitaja zawadi kwa timu itakayoibuka bingwa wa michuano hiyo kuwa ni pamoja na kombe, seti moja ya jezi pamoja na mipira mitatu na msindi wa pili atapata jezi seti moja na mipira miwili.