Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Nguvu zaidi ya kupima ardhi inahitajika

12th July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Jana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 siku moja tu baada ya Baraza la Mazingira nchini (Nemc)  ikishirikiana na wadau wengine wajibu wa ulinzi wa mazingira na matumizi sahihi ya ardhi kuvunja takribani nyumba 30 zilizojengwa kinyume cha sheria katika eneo la fukwe za bahari na mito ndani ya mita 60 jijini Dar es Salaam.

Hatua hizi za kwanza kuwahi kuchukuliwa kwa kiwango hiki. Ni hatua za ujasiri mkubwa kwamba inawezekana kushughulikia matatizo ya jeuri ya fedha ya kuvamia maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga ambayo kimsingi watu wamemilikishwa kwa njia za kona kona. Tunasema kungali mapema kwamba tunaunga mkono hatua hizi.

Itakumbukwa kwamba mara baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani Desemba 2005 miongoni mwa mambo ambayo Rais Jakaya Kikwete aliahidi kwa taifa katika hotuba yake ya kuzindua Bunge Desemba 30, mwaka 2005, ni kuchukuliwa kwa maamuzi machungu katika kulinda mazingira.

Rais aliahidi kuwa maamuzi hayo yangetangazwa na Makamu wa Rais Aprili mosi mwaka 2006, jambo ambalo lilitekelezwa na miongoni mwa maamuzi hayo ni kuondoa watu waliokuwa wamevamia maeneo oevu, vyanzo vya maji kama katika bonde la Ihefu mkoani Mbeya.

Kulikuwa na operesheni kabambe ya kuhamisha mifugo katika maeneo oevu ambako kisheria hairuhusiwi kulisha nchini kote.

Pamoja  na hatua hizo ambazo kwa hakika zilitikisa nchi nzima ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya nailoni yenye unene mdogo sana, kuanzisha taratibu mpya za ukataji mkaa na biashara ya magogo kwa ajili ya mbao kwa ujumla wake, tatizo la uvamizi wa maeneo ya wazi kwa ujenzi wa nyumba hakujapewa umuhimu wa kutosha hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.

Taarifa za serikali zinasema kuwa kuna viwanja zaidi 100 vilivyopo ndani ya hifadhi ya misitu ya mikoko kwenye fukwe za bahari na mito kinyume cha sheria katika jiji la Dar es Salaam pekee, hali hii pia ilikwisha kuelezwa na Waziri Tibaijuka ambaye alitoa hadhari kwa watu waliojenga nyumba zao ndani ya mita 60 kutoka ufukwe wa bahari na kwenye mito ikiwa ni mkakati wa kuokoa maeneo oevu na fukwe na kulinda mikoko kuangamia.

Kwa maana hiyo, operesheni ya juzi ya kubomoa nyumba hizo iliyoanza saa 1:00 asubuhi kwa kusimamiwa na polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi, ni utekelezaji wa maagizo ya siku nyingi ya serikali katika kulinda na kuhifadhi mazingira na kwa kweli kukomesha tabia ya watu kutumia ama nguvu ya fedha au ujeuri tu wa madaraka au kutokujua na kuvamia maeneo ambayo hayaruhusiwi kujengwa wala kumilikishwa mtu binafsi.

Kwa mfano, baadhi ya watu waliomilikishwa viwanja kinyume cha sheria tangu mwaka 2008 walionywa na Nemc wasijenge nyumba maeneo hayo, lakini walikaidi na kuendeleza ujenzi, pengine kwa kutumia nguvu ya fedha kupitia hasa Manispaa ya Kinondoni kulainisha upatikanaji wa vibali vya kujenga.

Tunasikitika kwamba kutokutii sheria na kutumia njia za mkato kupata viwanja kumewafikisha wananchi hawa waliobomolewa katika hasara kubwa ya kupoteza makazi.

Tunasema ni hasara kwa sababu hata kama mtu ana ukwasi mkubwa kiasi gani, kubomolewa nyumba ni hasara kubwa ambayo haipimiki.

Kuna hasara ya fedha, lakini pia kuna maumivu ya kisaikolojia yanayoshikamana na hisia za ndani juu ya mipango na malengo ya mtu hata kama bado ana fedha nyingi za kununua nyumba nyingine.

Pamoja na kutambua matatizo haya, pia tunatambua kuwa kuna udhaifu mkubwa wa upimaji wa ardhi/viwanja katika nchi hii.

Bado wananchi wengi hawana huduma hizi, wengi wanaojenga wanajenga tu katika maeneo ambayo wamejimilikisha kienyeji, hawana nyaraka, hayajapimwa hali ambayo inaibua changamoto kubwa sana ya maendeleo ya makazi.

Kwa mfano, ni chini ya asilimia 20 tu ya makazi yote ya Dar es Salaam ndiyo yamepimwa; kwingineko kila mtu na juhudi zake binafsi, hali hii inakwaza mambo mengi sana ya maendeleo kwa wanaomiliki nyumba na hata mashamba.

Tunafikiri pamoja na msuli huu wa serikali wa kubomoa nyumba za waliovamia maeneo yasiyoruhusiwa, ni wakati sasa umefika kwa kuelekeza nguvu zaidi katika operesheni ya kupima ardhi yote ya taifa hili na kutayarisha hati zake.

Hali hii itakomesha maumivu tunayoshuhudia kwa wakazi wenye nyumba hizi 30 za Dar es Salaam.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment