


.jpg)
.jpg)
.jpg)
Timu nne za Tanzania zitakutana katika robo-fainali ya Kombe la Kagame la klabu bingwa ya soka ya Afrika mashariki na kati kesho na keshokutwa, baada ya Simba na Azam jana kutoka sare katika mechi zao za mwisho za hatua ya makundi.
Sare ya bila kufungana ya Azam dhidi ya Tusker ya Kenya kwenye Kundi B mchana ilimaanisha kuwa wauza vyakula hao wanamaliza kileleni mwa msimamo licha ya kufungana kwa pointi na magoli na Mafunzo ya Zanzibar, hivyo kuikwepa Yanga iliyoshika nafasi ya pili ya Kundi C juzi kwa kuifunga APR ya Rwanda 2-0.
Lakini penalti iliyopotezwa na Felix Sunzu katika dakika za mjeruhi jana kwenye Uwanja wa Taifa pia katika mchezo wa jioni, ilisababisha Simba ishike nafasi ya tatu kwenye Kundi A na hivyo kuangukia kwa Azam katika hatua ya timu nane bora.
Wakati Yanga itaikabili Mafunzo kesho, Azam na Simba zitakutana katika mchezo wa pili wa robo-fainali keshokutwa, baada ya pambano kati ya URA na APR.
Atletico ya Burundi na Vita ya JK Kongo zitafungua hatua hiyo kesho kabla ya wenyeji hao kukutana.
Kocha wa Simba Milovan Cirkovic alisema mchezo dhidi ya Azam utakuwa mgumu lakini ana matumaini ya kushinda kutokana na marekebisho anayotaraji kufanya kutokana makosa ya jana.
Mwalimu msaidizi wa Vita ambayo imeonyesha soka la kuvutia kwenye michuano hii kama ilivyo kwa Atletico, Raul Shungu ambaye aliwahi kuifundisha Yanga mara mbili huo nyuma alisema timu hiyo ya Burundi ni nzuri lakini kwasababu wanaifahamu haitawasumbua.
"Simba ni wazuri lakini wana tatizo kubwa la kupoteza mipira na nafasi za kufunga," alisema Shungu.
Ukiacha kosa la penalti, Simba kama Vita yenyewe ilipoteza nafasi nyingi za hatari katika mchezo huo uliokuwa wa kuvutia.
Goli la Vita lilifungwa kwa penalti na Etekiama Taddy katika dakika ya 34 baada ya Juma Nyoso kunawa mpira ndani ya eneo la hatari akiwa katika harakati za kuokoa.
Haruna Moshi 'Boban' aliingia kutoka benchini na kuunganisha kwa shuti maridadi krosi ya beki mbili Musa Mude kutoka wingi ya kulia katikati ya kipindi cha pili.
Azam imefungana na Mafunzo ya Zanzibar kwa magoli na pointi kufuatia sare baina yao ya 1-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini inakaa juu ya msimamo kutokana na kuwa ilitangulia kupata bao hilo.
Katibu mkuu wa wenyeji wa Kombe la Kagame, shirikisho la soka, TFF, Angetile Osiah aliiambia Nipashe jumapili jana kuwa kanuni zinataka mshindi aamuliwe kutokana na matokeo baina ya timu uwanjani.
"Katika mchezo baina ya timu hizi, Azam walitangulia kufunga kwahiyo wao ndiyo wataongoza na Mafunzo ni ya pili. Hivyo ni Yanga na Mafunzo Jumatatu (kesho)," alisema Osiah.
Kocha wa Azam Stewart Hall alisema baada ya mchezo kuwa tatizo la timu yake ni kuwa haijafika katika kiwango chake cha ubora wa kasi hivyo kutotengeneza nafasi nyingi za magoli kama kawaida yake.
Lakini, pamoja na kutopigiana pasi fupi-fupi kwa kasi kama wanavyotaka, pia inapoteza nafasi nyingi za kufunga kati ya chache inazopata, alisema.
"Usisahau kuwa Azam imegonga mwamba mara tatu katika mchezo huu," Hall alikiambia kituo kimoja cha televisheni mara baada ya mchezo.
Simba na Azam zilitoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa mwisho baina yao, fainali ya Kombe la Urafki wiki mbili zilizopita lakini Wekundu wa Msimbazi ni mabingwa wa michuano hiyo kufuatia ushindi wa matuta.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Juma Kaseja, Juma Shamte, Obadia Mungusa, Juma Nyoso, Musa Mude, Amri Kiemba (Salum Kinje dk.70), Mwinyi Kazimoto, Nkanu Mbiyavanga (Haruna Moshi dk.45), Felix Sunzu, Danny Mrwanda, Kigi Makasi.