


Yapo mambo mazuri ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano linayatekeleza katika kutimiza wajibu wake kwa umma. Ni wajibu wake kufanya hivyo.
Lakini yapo mambo mengine yasiyokuwa na tija kwa umma, yanayofanywa na wabunge na wakati mwingine mawaziri.
Wanaoyafanya mambo yasiyokuwa na tija kwa umma ndani ya Bunge, wanapotosha, wanalaghai, wanakera.
Ingawa ni hivyo, wapo wabunge na mawaziri wanaozigusa hisia na matarajio ya umma. Wanatimiza wajibu wao kwa umma. Wanajenga, wanawasilisha, wanasimamia maslahi ya umma.
Vikao vya Bunge la bajeti vinaendelea, huku wizara zikiwasilisha mapendekezo ya mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.
Katikati ya hali hiyo, michango na hoja za baadhi ya wabunge na mawaziri inasikitisha, ni kama wanafanya mzaha, hawatambui umuhimu wa bajeti na athari zake kwa umma.
Bajeti ni tukio lisilohitaji mzaha, linahitaji umakini katika kuijadili, kwa maana ni msingi mkubwa katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya nchi na ustawi wa watu wake.
Hilo linaonekana kutokuwa sehemu ya hisia za baadhi ya wabunge na mawaziri. Wanafikiria maslahi ya kisiasa, wanavipigia debe vyama vyao na kuiacha jamii huru ya Watanzania inayosubiri kujikomboa kupitia bajeti hiyo. Mathalani akijibu hoja za wabunge katika kuhitimisha bejeti ya wizara yake, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alionekana kujikita zaidi katika hoja za kisiasa, akikipigia debe Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Binafsi nilijiuliza, hivi kero zinazoikabili jamii pana, zinawaepuka wanachama na wafuasi wa CCM, kiasi cha kuwashawishi baadhi ya wabunge na mawaziri kushindwa kujikita katika ukweli na kubaki ‘kupiga siasa’ kwa jambo nyeti kama bajeti?
Kwa mfano, alijibu hoja za wabunge, Magufuli ambaye ni mmoja wa mawaziri wanaoaminika kwa utendaji kazi bora, akasema fedha za CCM ndizo zinatumika kushughulikia maendeleo ya nchi. Inasikitisha.
Hivi katika hali ya kawaida, inakuwa vipi kiongozi kama Magufuli kutoa kauli hiyo, tena ndani ya chombo cha uwakilishi wa umma, akilidanganya Bunge huku akipigiwa makofi na wabunge wanaoaminika kuwa wanachama wa CCM?
CCM ina hela gani, zinatoka wapi na kwa sheria ipi inatumika kuipa mamlaka ya kushughulikia maendeleo na ustawi wa jamii? Ulaghai mtupu!
Fedha za maendeleo na ustawi wa jamii zinatengwa na serikali ambayo licha ya kuundwa na CCM, ni mali ya umma. Fedha zinazotengwa na serikali hazitokani na ada za uanachama wa CCM ama chanzo kingine chochote ndani ya chama hicho, bali kodi za wananchi. Kupiga propaganda ya kutaka kuuaminisha umma kwamba fedha za maendeleo na ustawi wa jamii ni za CCM, haionyeshi dhamira madhubuti ya kushughulikia kero za jamii.
Ni mzaha ndani ya Bunge, ni kituko ndani ya Bunge, ni kulidhalilisha Bunge lipoteze mamlaka ya uadilifu katika kutimiza wajibu wake.
Tanzania hivi sasa inazungumzia kupiga hatua za maendeleo na ustawi wa watu wake, kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi, maisha ya wananchi wanaboreka.
Watawala wanapaswa kuwa sehemu ya kuchagiza kasi ya wananchi kujiona kuwa ni sehemu muhimu katika kufikia azma ya kukuza uchumi, kuchagiza maendeleo na kuistawisha jamii.
Moja ya mambo yanayopaswa kufanywa ni kurejesha ari ya uwajibikaji wenye kukidhi vigezo vya uadilifu uliotukuka. Uwajibikaji na uadilifu vitafanikiwa kwa urahisi ikiwa kila raia atatambua nafasi yake katika kumiliki, kulinda na kuzitetea rasilimali za umma.
Kuzitangaza fedha za umma kuwa mali ya CCM ni upotofu unaoweza kutafsiriwa kama sehemu ya kukibeza chama hicho, kwa maana ukweli wake haupo hivyo. Bunge letu linapaswa kuheshimiwa, ushabiki wa vyama vya siasa usiwe sehemu ya kufifisha dhana ya maslahi ya umma ili nchi ifikie hadhi ya kuwa na maendeleo endelevu.
Vyama vya siasa vipo, vikiwa na wanachama wanaojiunga kwa nia na kusudio tofauti, lakini taifa na kizazi chake vinapaswa kuwa juu ya vyama hivyo.
Hivyo nchi ‘inapoelekea’ bungeni mjini Dodoma, wabunge na mawaziri wanapaswa kujiweka kando ya mizaha inayoweza kugeuza taswira ya vikao vya bajeti kuwa mfano wa michezo ya kuigiza ama ya kufurahisha maarufu kama ‘comedy’.
Mawaziri na wabunge watambue umuhimu wa kuwepo kwao bungeni na wajibu wanaopaswa kuutelekeza, wakihoji maswali ama kutoa majawabu yenye mashiko kwa umma.
Kwa mfano hoja kama inayoelekezwa katika kuwepo bajeti zinazojumuisha fedha nyingi zitakazotumika kulipa madeni badala ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Ama miradi kama ya ujenzi wa barabara kupewa fedha zinazoweza kukidhi ujenzi wa kambi ya wajenzi na si ujenzi rasmi, vinapaswa kujadiliwa kwa uzito stahili.
Kwa maana hali ilivyo, ni dhahiri kwamba siasa inapoingizwa katika mambo yenye maslahi kwa umma, inakuwa ishara ya ukomo wa fikra zilizopo katika kuitumikia nchi.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa ambaye hivi sasa yupo bungeni mjini Dodoma. Anapatikana kwenye simu namba +255 745 691540, 0716635612 ama barua pepe;mgeta2000@yahoo.com.