Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wapinzani walipua vigogo bungeni

21st July 2012
Print
Comments

Kambi ya Upinzani Bungeni imewalipua vigogo watano wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiwemo wabunge wawili wa chama hicho kuwa waligawa Sh 7,325,000 kama posho ya kikao kimoja cha  Bodi ya Korosho nchini.

Wabunge waliolipuliwa ni Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, aliyekuwa Mbunge wa Mchinga (CCM), Mudhihir Mudhihiri na mkewe.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili, aliyasema hayo bungeni jana wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13.

Alisema Bodi ya Korosho imekuwa ikiwanyonya wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma kwa kujilipa posho nyingi na marupurupu mengine huku wakiwaacha wakulima wa korosho wakiteseka na kuhangaika huku na huko kama kondoo wasio na mchungaji bila kutatua matatizo yao.

Alisema kuwa bodi hiyo ilipokea shilingi bilioni mbili kati ya Oktoba mwaka jana na Januari mwaka huu, kutokana na ushuru wa mazao ya nje ya korosho kwa msimu wa 2010/2011.

Alisema  Kiasi hicho kilikuwa ni kwa ajili ya shughuli za kuendeleza tasnia ya korosho nchini.

Hata hivyo, alisema kwa masikitiko makubwa fedha hizo hazikutumika kufanya shughuli kama ilivyotarajiwa na badala yake zilitumika kugharamia vikao vya bodi ya wakurugenzi na safari za viongozi (management ya bodi) ambazo hazijaleta tija kwa tasnia nzima kama ilivyokusudiwa.

Alisema kwa kikao cha siku moja kilichofanyika Noveba 29, mwaka jana, wajumbe wa bodi hiyo walilipwa posho mbalimbali kulingana na wadhifa wao.

Alisema Bwanausi ambaye ni Mjumbe wa Bodi hiyo  alilipwa Sh 1,550,000 ikiwa ni Sh 750,000 kama posho ya kawaida (Per diem) na sh 800,000 ni “working session” kama ilivyoandikwa kwenye fomu ya malipo.

Mwingine ni Anna Abdallah kama mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi alilipwa jumla ya Sh 1,800,000,  ikiwa ni posho ya kikao Sh 500,000,  usafiri Sh 300,000, posho ya kawaida Sh 900,000 na usafiri wa Dar es Salaam Sh 100,000.

Kamili alimtaja pia Bwanausi kama mmoja wa wakurugenzi ambaye alilipwa kwa mara nyingine tena kwenye kikao hicho hicho jumla ya Sh. 1,550,000 ikiwa posho ya kikao ni Sh. 400,000, usafiri wa ndege Sh. 300,000, posho ya kawaida Sh 750,000 na usafiri Dar es Salaam Sh 100,000.

Alimtaja mjumbe mwingine wa bodi hiyo ambaye alilipwa kiasi kikubwa katika posho hiyo kuwa ni  Mudhihir aliyelipwa Sh 1,550,000 ikiwa na posho ya kikao ni Sh. 400,000, usafiri wa ndege Sh. 300,000, posho ya Kawaida Sh. 750,000, usafiri Dar es Salaam Sh. 100,000.

Kamili alimtaja mwingine kuwa ni mke wa Mudhihir ambaye aliyelipwa Sh 875,000 ikiwa ni posho ya kikao Sh. 200,000, usafiri Sh  300,000, posho ya kawaida Sh. 375,000.

“Jumla ya fedha zote zilizolipwa (kwa watu watano)  katika kikao hiki cha wakurugenzi wa Bodi ya Korosho cha tarehe 29/11/2011 ni shilingi  7,325,000,”alisema Kamili.

Alisema licha ya matumizi ya fedha hizo kuwa hayana tija kwa kuwa matatizo ya wakulima wa korosho hayajapatiwa ufumbuzi hadi sasa, utaratibu walioutumia wajumbe hao kujipatia fedha hizo una dalili za kifisadi ndani yake.

Alihoji kuwa mke wa Mudhihir ambaye si mjumbe wa kikao aliingia kwenye kikao na kulipwa posho na utaratibu uliotumika kumlipa mke wa Mudhihir haueleweki na hata viwango vilivyotumika kukokotoa malipo yake pia havifahamiki.

“Dalili ya ufisadi mwingine katika bodi hii, ni kwa Mjumbe wa bodi Mh. Jerome Bwanausi kulipwa posho hiyo mara mbili.

Katika fomu za malipo kwa Mh. Bwanausi, fomu moja ameandika jina lake kwa kifupi yaani J. Bwanausi na tarehe ya kuchukua fedha ameandika ni tarehe 28/11/2011 wakati katika fomu ya pili ya malipo ameandika jina kamili yaani Jerome Bwanausi na tarehe ya kuchukua fedha kaandika 29/11/2011,”alisema.

Alisema mazingira kama hayo, yanaibua hisia kuwa  Bwanausi alijipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu na hivyo kuwaaminisha watu kuwa alitumia nafasi yake kama mjumbe wa bodi ya korosho  kuchukua fedha za wakulima wanyonge wa korosho.

Akisoma hotuba ya bajeti yake, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alisema jumla ya tani 31,000 zilibanguliwa hapa nchini ikiwa ni asilimia 19 ya korosho zilizozalishwa.

“Maandalizi ya ujenzi wa viwanda viwili vya Tanecu Ltd na Perfect Cashew Kernel vyenye uwezo wa kubangua tani 32,000 yanaendelea,”alisema.

Aidha, alisema kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), ilifanya tathimini ya viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa.

Alisema taarifa ya tathimini hiyo inaonyesha kuwa baadhi ya viwanda hivyo haviendeshwi kulingana na masharti ya ubinafsishaji.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment