Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kampuni 1,935 kushiriki Maonyesho ya Sabasaba

21st June 2012
Print
Comments

Kampuni 1,935 kutoka ndani na nje ya nchi zinatarajia kushiriki katika maonyesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yatakayoanza rasmi Juni 28 hadi Julai 8 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Billy Mvingira, alisema maandalizi yanaendelea vizuri na tayari nchi 11 zimethibitisha kushiriki maonyesho hayo ambayo yatazinduliwa rasmi Julai Mosi na mgeni rasmi atakayetajwa baadaye.

Akifafanua Mvingira alisema kati ya kampuni zitayoshiriki, 435 ni kutoka nje ya nchi na makampuni 1,500 ni ya ndani ya nchi, huku taasisi 64 za serikali zikithibitisha kushiriki.

Aidha, Mvingira alizitaja baadhi ya nchi zitakazoshiriki ni Rwanda na China ambazo zimechukua eneo kubwa katika viwanja hivyo, nyingine ni Kenya, Msumbiji, Syria na Sudan.

Alisema viingilio kwa watoto vitakuwa Sh. 500 na watu wazima 2,500 katika siku zote za maonyesho hayo isipokuwa siku ya kilele chake Julai 7 ambapo viingilio vitaongezeka kwa watoto sh.1,000 na watu wazima Sh. 3,000.

Mvingira aliwataka wafanyabiashara hapa nchini kuchangamkia kushiriki katika maonyesho hayo kwa kuwa ni fursa pekee ya kujitangaza, kukutana na wadau wao ambao watawapa maoni mbalimbali na kuweza kuboresha bidhaa zao.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment