Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Makamba awe wa kwanza kushughulikiwa CCM

17th June 2012
Print
Comments
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, January Makamba

Nimesoma baadhi ya magazeti kwenye matoleo ya jana, moja ya habari iliyonivutia ni kumhusu Naibu Waziri wa Nishati na Madini, January Makamba, kutaka baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) washughulikiwe.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM mjini Dodoma, zimemkariri Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga, akisema wabunge hao ni wale waliosaini waraka wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe.

Lengo la waraka huo lilikuwa kukidhi vigezo vya kanuni za Bunge, ili hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, ijadiliwe na hatua kuchukuliwa.

Hoja hiyo ilitokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Kamati ya Bunge ya Mazingira, Ardhi na Maliasili, kubainisha ‘uozo wa kutupwa’unaojikita katika ubadhirifu wa mali za umma.

Taifa na dunia kwa sehemu kubwa, iliunga mkono msimamo wa wabunge hususani waliomo ndani ya CCM. Rais Jakaya Kikwete aliyemteua Makamba kushika wadhifa huo, pia aliunga mkono.

Niliposoma habari hiyo, nikakumbuka kisa cha aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, alipowahi kupendekeza viongozi waliosababisha CCM ishindwe kwenye baadhi ya maeneo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Niliandika makala ya uchambuzi kuhusu hatua ya ‘Makamba mkubwa’ na ambayo ninaamini ingawa kuna tofauti za mazingira ndani ya chama kile kile, `Makamba mdogo’ anaweza kujifunza kutoka hapo.

Ninairejea makala ya uchambuzi niliyoiandika Januari 12, mwaka jana, ikabeba kichwa kinachosema ‘Makamba awe wa kwanza kutimuliwa CCM’. Inaweza kutoa picha ya hali ilivyoripotiwa kwenye magazeti ya jana.

Iliandikwa hivi:

MAPEMA wiki hii, nilifikiria namna bora ya kukishauri Chama Cha Mapinduzi (CCM), kijiboreshe ili kufikia matarajio ya umma.

Nilitaka kuizungumzia CCM kama ninavyoizungumzia sasa, kutokana na ukweli kwamba ndicho chama tawala, kipo madarakani, kinapendwa, kimewasilisha ilani ya uchaguzi iliyo miongoni mwa misingi wa sera, mipango na mikakati ya maendeleo ya taifa.

Moja ya eneo kubwa nililotarajia kuliweka bayana katika Mtazamo Yakinifu, ni kuwashughulikia viongozi wasiofaa na ambao utendaji wao unaliingiza taifa katika matukio ya aibu.

Utendaji wa baadhi ya viongozi wa CCM umekuwa chachu ya machafuko. Mazingira yanaashiria kuwa baadhi ya watendaji serikalini, wakiwemo Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa, majiji na makamanda wa polisi katika ngazi tofauti, wamejikuta katika shinikizo la kisiasa.

Hali hiyo inajitokeza kupitia mgongo wa `chama kimesema’, na kutokana na mfumo wa kiutawala, wanaoshinikizwa wanashindwa kuhoji, bali kutekeleza, basi!

Kama ni kupiga raia wasiokuwa na hatia ili kutekeleza agizo la `chama kimesema’-watawapiga, ikibidi wajerUhiwe ama vinginevyo!

Lakini unaporejea katika uhalisia wake, si kweli kwamba `chama kimesema’, bali viongozi wasiokuwa na sifa, wasiokuwa na uwezo, wanaobebwa kwa sababu za `huyu ni mwenzetu’, wanakiharibu chama hicho, wanaiharibu nchi. Wanaongeza hasira za wananchi kuichukia CCM.

Zipo sababu kadhaa ambazo kama chama cha siasa, hata kama kipo madarakani, wanapovurunda, wanaowajibika ni viongozi wake, kuanzia ngazi ya taifa hadi chini katika jamii.

Mfano mzuri (japo kwa kujiuzulu) ni wakati chama tawala cha Republican nchini Marekani, kiliposhindwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea kupitia chama pinzani (wakati huo) cha Democrat, Barack Obama (Rais) alishinda. Kama ingekuwa ni `wendawazimu’ wa kutumia dhana ya `chama kimesema’, bila shaka Rais aliyekuwa anamaliza muda wake, George Bush, angeyaamuru majeshi ya ulinzi na usalama, kuhakikisha Republican inarejea madarakani.

Haikuwa hivyo. Aliyekuwa mgombea kupitia Republican katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba 4, 2008, John McCain na timu yake, walishindwa vibaya na Obama akawa Rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika nchini humo.

Hali kama hiyo ilitokea nchini Uingereza, ambapo Waziri Mkuu aliyekuwa madarakani, Gordon Brown alishindwa na mpinzani wake, David Cameron, katika Uchaguzi Mkuu wa Mei 6, mwaka jana.

Nchini Kenya, ukiacha machafuko yaliyotokea mwaka 2007, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002 ulishuhudia Mwai Kibaki aliyegombea urais kupitia NARC, akimshinda Uhuru Kenyatta wa kilichokuwa chama tawala cha Kanu. Ikawa hivyo. Upo mlolongo wa mifano unaoweza kutumika ili kuhalalisha hoja hii, lakini katika ujumla wake, ililenga kuepuka dhana ya `chama kimesema, kiti hicho lazima kirejee CCM’.

Nani kasema CCM ni mlezi mkuu wa taifa hili lililopata uhuru wake Desemba 9, 1961? Nikiwa katika kutafakari juu ya ushauri huo, ninalisoma gazeti hili katika toleo lake la Januari, 10, mwaka huu. Ninakutana na karipio la Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

Makamba ambaye ni sawa kusema kuwa CCM `inamfia’ mikononi, anapata ujasiri wa kutamka, kwa kinywa chake, kwamba viongozi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao, waondolewe ndani ya chama hicho.

Hivi ni nani aliyestahili kuwa mfano wa wanaostahili kuwekwa katika orodha ya uwajibikaji ndani ya CCM kati ya Makamba na viongozi waliopo chini yake?

Sina chuki na Makamba kwa namna yoyote, lakini linapokuja suala la maslahi ya umma, CCM ikiwa moja ya taasisi za jamii, haipaswi kwa Katibu Mkuu ambaye `chama kimemshinda’ akawatupia mpira waliopo chini yake!

Chama kimepoteza viti vingi vya ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, udiwani na hata kushuka vibaya kwa asilimia za kura za mgombea urais wake. Yeye bado anajiweka kuwa miongoni mwa viongozi bora?

Mkutano wa Makamba katika uzinduzi wa Mishemishe group pale Kariakoo jijini Dar es Salaam, ulinishtua hasa kupitia tamko hilo. CCM inapaswa iepuke woga, ichukue uamuzi mgumu wa kuwashughulikia viongozi wasiokuwa na uwezo kuanzia ngazi ya taifa. Kwa maana, hatua ya kuwalea viongozi wa aina hiyo, imekuwa chanzo cha shinikizo la kisiasa kwa watendaji kama wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa na majiji ama watumishi wakiwemo makamanda wa polisi, kuihujumu demokrasia, uhuru na haki za raia.

Viongozi wasiofaa ndani ya CCM wanatumia janja ya `chama kimesema’, ili kulinda udhaifu wao, uwezo wao duni na ukosefu wa maono ya uongozi katika kuifikia dira ya maendeleo ya taifa hili.

Pamoja na heshima nilizonazo kwa Makamba, ninaamini kwamba alistahili kuwa mfano bora, kwamba baada ya kushindwa uongozi, angewajibika ama vinginevyo awe wa kwanza kung’olewa ili hadhi, heshima na mashiko ya CCM yarejee kwa wananchi.

Hivi CCM inasubiri mpaka ibaki na viti (mathalani) vitano kwa Tanzania Bara na kimoja kwa Zanzibar, ndipo iamini kuwa ikiwa chini ya Makamba, hakuna mafanikio yoyote? Lazima CCM izinduke na kutambua kwamba kumshughulikia Makamba hakuna athari yoyote kwa vile hatua hiyo itagusa wadhifa wake akiwa Katibu Mkuu, lakini atabaki kunufaika na haki nyingine akiwa miongoni mwa raia zaidi ya milioni 40 wa Tanzania.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE Anapatikana katika simu namba +255754691540, +254702115303 au barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment