Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Bajeti haina dhamira kuinua Watanzania

16th June 2012
Print
Comments
Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa

Siku mbili baada ya serikali  kutangaza bajeti ya Sh trilioni 15 wananchi wameendelea kuibeza kuwa hailengi kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2012/13 umejaa mashaka kwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya  fedha za maendeleo ya nchi zinategemea misaada, mikopo na hisani za wafadhili.

Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa, alisoma bajeti hiyo bungeni juzi akibainisha serikali itatumia  Sh. trilioni 15  ambazo trilioni 4.5 zimetengwa kwa ajili ya maendeleo.

Lakini kati ya hizo trilioni 4.5 Tanzania inategemea trilioni 2.3  zaidi ya nusu zitolewe na wafadhili jambo linalifanya taifa tegemezi kwa fedha za nje kujiletea maendeleo.

Iwapo wafadhili hawatatoa mikopo na misaada kwa wakati  Tanzania itashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyokusudiwa.

Pia iwapo watagoma kusaidia nchi itashindwa kujiletea maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2012/13.

Bajeti ya matumizi ya maendeleo ni Sh trilioni 4.5 kati ya hizo fedha za wahisani ni trilioni 2.3 na kiasi kilichobakia cha trilioni 2.2 ni pesa zinazotoka kwenye Hazina ya Serikali.

Hata hivyo, bajeti hiyo yenye karibu kurasa 100 haielezi mikakati ya kupunguza matumizi makubwa ya serikali ambapo zaidi ya asilimia 70 ya bajeti yote ni kulipana mishahara, kununua vitafunio, magari, safari za  ng’ambo, kulipa kodi  na shughuli zote za utawala maofisi.

Akiichambua,  Meya wa zamani wa Dodoma, Peter Mavunde alisema  Waziri Mgimwa anatakiwa kuweka uwiano wa bajeti ya fedha za matumizi ya  shughuli za kila siku na fedha za maendeleo na kurekebisha uwiano huo wa kutenga  fedha kiduchu za maendeleo.

Alishauri kuorodhesha matumizi yote na kuangalia yale yasiyo na umuhimu ili fedha zake zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na kuongeza kuwa nchi haiwezi kuendelea kama haitapunguza matumizi makubwa ya serikali na kupeleka fedha kwenye maendeleo.

Alisema; “ule utashi wa kuwaletea watu maendeleo hauonekani katika bajeti hii. Sioni sababu serikali isionyesha jinsi ilivyokusudia kupunguza matumizi ili itumie fedha nyingi kwa maendeleo.

Mfano itangaze kuacha kutumia magari ya kifahari, ijifunze kutoka kwa wenzetu jinsi wanavyopunguza matumizi makubwa ili kujiletea maendeleo”

“Tuchambue matumizi makubwa yasiyokuwa na maana na kuangalia hivi kama  tutaondoa magari ya kifahari, safari za ng’ambo , posho zisizo za lazima mtu atashindwa kutimiza wajibu…?”

Anasema hakukuwa na sababu za kuanzisha wilaya na mikoa mipya kwani inaongeza  gharama zisizokuwa na umuhimu  kwa vile  majukumu ya wakuu wa mikoa (RC) na wilaya  DC yamechukuliwa na serikali za mitaa.

Wakichangia maoni, wakazi wa Dodoma hasa wajasiriamali wadogo walimuunga mkono Meya huyo na kueleza kuwa bajeti haijaainisha dhamira ya kupunguza matumizi makubwa ya kuendesha serikali.
 
Kadhalika walisema licha ya kuanisha mipango ya kuongeza ajira kwa vijana  kwa kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)   tatizo la kutegemea fedha za wafadhili  ili kutimiza malengo hayo linawafanya kukosa  matumaini.

Kadhalika kwenye elimu imeanisha masuala ya kuboresha kiwango cha elimu, mafunzo kwa walimu wa Sayansi na kuongeza ajira za walimu wa shule za kata na katika huduma za afya lakini ni mipango isiyo na uhakika kwani fedha zake hazina uhakika wa kupatikana kwani ziko mikononi mwa wafadhili.

Kwa upande mwingine bajeti haikutoa unafuu wa kuzalisha umeme hasa kwa kutumia mafuta mazito ya kuendesha mitambo ili kulisaidia Shirika la Umeme  (Tanesco) kupunguza bei ya umeme. Watanzania walitarajia serikali kupunguza kodi za mafuta mazito ya kuzalisha umeme kwenye mitambo mfano  IPTL lakini bajeti imebakia kimya .

Pia ingeondoa kodi za vipuri na vifaa  vya kuunganisha  umeme vinavyoagizwa nje na Tanesco ili kupunguza gharama lakini bajeti ya serikali imekuwa bubu kwenye eneo hilo na kuacha mzigo wa gharama za umeme zinazopandisha bei za maisha kuendelea kuumiza Watanzania. Licha ya kutangaza kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, kwa mwaka huu wa fedha.

Kwa mujibu wa ukurasa wa 64 na 65 wa kitabu cha bajeti, serikali imeondoa ushuru kwa mafuta mazito ya kuendesha mitambo,  bila kuzungumzia  msamaha kwa Tanesco.
 
Bajeti hiyo iliyosomwa bungeni juzi haikuzungumzia lolote kuhusu kodi za mafuta licha ya kwamba wasafirishaji wakiwemo wa daladala jijini Dar es Salaam na maeneo mengine mikoa wanatishia kupandisha nauli kutokana na ughali wa mafuta.

Gharama za mafuta zimechangia ongezeko kubwa la bei za vyakula kutokana na usafiri kutoka mashambani hadi sokoni kuwa wa juu lakini bajeti haikutaja lolote juu ya kurekebisha kodi sumbufu za mafuta.

Kwa upande wao, viongozi wa Kanisa la Pentekoste Holiness Association Missions (PHAM), la Dodoma walisema bajeti ya serikali haijawasaidia wafanyakazi kwa kuwa imeongeza kodi ya mshahara (PAYE).

Katibu wa Askofu wa  PHAM , Julius Bundala , alisema bajeti imewaumiza zaidi wafanyakazi wanaotegemea mshahara kwa asilimia mia moja na kushauri kuitizama upya ili kuondoa migogoro na wafanyakazi .

 Pia alisema oongezeko la mikoa na wilaya limesababisha bajeti kuwa juu  bila sababu na kuongeza kuwa uongezwaji wa maeneo makubwa ya utawala ni mambo yanayotakiwa kuachwa badala yake kuongeza fedha za kuleta maendeleo.

SINGIDA WAMEIPOKEAJE?

Baadhi ya wananchi mkoani Singida wamepokea kwa mtizamo tofauti Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni, kwa madai kuwa itaaathiri wafanyabiashara wadogo na wa kati wasiopenda kuweka kumbukumbu za biashara zao.

Wamesema kuwa, wafanyabiashara wadogo sasa watakutana na ushuru mwingi wa aina tofauti tofauti, ambao utatoa fursa kwa halmashauri kuwabana kwa kuwatoza ushuru mbalimbali.

Wakiongea na NIPASHE Jumamosi, wananchi hao Cathbert Nkurlu, Juma Mudida, Saad Mhando (Mangala) na mwalimu Tabu Mohammed, walisema kwa ujumla serikali iwapo itatekeleza bajeti hii, itasaidia kwa kiasi fulani kutatua kero mbalimbali.

Aidha wameeleza kushangazwa na ukimya wa serikali kushindwa kuzungumzia kodi ya kuku na mayai, biashara ambayo inawaingizia watu wengi kipato kikubwa kiasi cha kumudu maisha na kuwatajirisha watu wengi.

Kwa ujumla pamoja na dosari zilizojitokeza, bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni nzuri…serikali tu ijipande vizuri katika kuitekeleza, kama ilivyosomwa, hapo naamini itasaidia kumkomboa mwanachi wa kawaida,”alisema Nkurlu.


 
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment