


.jpg)
Kamati ya Sheria na hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la soka (TFF) imesema Yanga ipo shahii kumtumia beki Kelvin Yondan katika mashindano yanayoendelea sasa ya Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, baada ya kubaini mkataba wa Simba na mchezaji huyo sio sahii.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema kamati yake ilikutana Julai 17 kupitia mikataba na nyaraka zote za Yondani na kutuoa umauzi.
Mgongolwa alisema kwa mujibu wa mapitio ya nyaraka za Yondani, kamati ilibaini kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Simba ulimalizika Mei 31 hivyo kwa taratibu za usajili Yondani alikuwa huru kuanzia Juni mosi mwaka huu.
"Aidha Kamati ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya hiyo uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda wake," alisema.
"Hivyo mkataba huo mpya wa Simba na Yondani kwa jicho la kisheria haupo," alisema Mgongolwa.
Aidha, alisema kuwa hata kama kamati yake ingeuona mkataba huo upo katika jicho la sheria, bado mkataba huo una matatizo kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano hayo.
"Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana uliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey Nyange Kaburu, Desemba 23 mwaka huu," alisema Mgongolwa.
Aidha, alisema, kisheria utata wa mchezaji huyo unaweza kuondolewa na pande husika kwa kurekebisha dosari hiyo kwa maridhiano na kuweka saini katika mabadiliko hayo.
Hivi karibuni TFF kupitia kwa katibu wake, Angetile Osiah, ilimuidhinisha Yondani kuchezea Yanga kwenye mashindano ya Kagame kitendo ambacho uongozi wa Simba ulilalamika kwa madai kuwa mchezaji huyo amesajiliwa na klabu yao.
Maamuzi hayo ya kamati ya Mgongolwa yatakuwa pigo kwa Simba ambayo imeendelea kushikilia msimamo kuwa beki huyo wa kati ni mchezaji wake halali baada ya kuingia naye mkataba mpya Desemba 23 mwaka jana.