



Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewataka wajasiriamali wa kati na wadogo nchini wawe waangalifu na makini katika biashara wanazodhamiria kuzifanya kama kweli wanataka kufanikiwa maishani na akawaonya wale waliopata mbegu mtaji kuchukua tahadhari zaidi.
Alitoa onyo hilo jana wakati akizungumza na wajasiriamali kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambao walihudhuria sherehe za kutoa zawadi kwa washiriki wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (Business Development Gateway - BDG) kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Naomba niwatahadharishe kuwa ujasiriamali unataka umakini wa hali ya juu. Mmoja wa Wajasiriamali mashuhuri huko Marekani aliwahi kutoa tahadhari kwa kusema: "Business is like oil, it won't mix with anything but Business", akimaanisha kwamba (biashara ni kama mafuta ya kulainisha mitambo ambayo hayachanganywi na kitu kingine chochote).
Tunahitaji uangalifu na umakini katika kufanya biashara zetu bila kuchanganya na mambo mengine," alisema. Amesema mtu anapochukua mkopo kwa nia ya kuanzisha biashara kisha akaamua kuoa mke wa tatu au kununua gari kwa kutumia fedha hiyo ya mtaji ni lazima atakwama kwa sababu atakuwa amechakachua dhima nzima ya ile biashara yake.
Alisema katika mabanda ya maonyesho aliyotembelea leo, ameona changamoto kuu tatu ambazo zinahitaji kuangaliwa haraka ili kuinua soko la bidhaa za wajasiriamali hao.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa vifungashio bora, ukosefu wa alama za viwango kutoka shirika la viwango nchini (TBS) na ukosefu wa alama ya biashara (bar code) katika bidhaa zao.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Bi. Esther Mkwizu alisema jumla ya washindi 1,570 kutoka mikoa yote wamepatiwa tuzo ambayo ni mbegu mtaji yenye thamani ya sh. bilioni 5.75.